CONTE AMPA DIEGO COSTA KAZI YA KUPACHIKA MABAO 30 CHELSEA MSIMU HUU

KOCHA wa Chelsea, Antonio Conte amempa kibarua straika wake, Diego Costa kuhakikisha msimu huu anafunga mabao 30 ikiwa ni baada ya kumvimbisha kichwa akimsifia kipaji chake.

Costa ndie aliyekuwa tegemeo kwa upachikaji mabao kwenye michuano ya Ligi Kuu msimu wa 2014/15 lakini akaja kugeuka “kiraza” msimu uliopita wakati vinara hao wa Stanford Bridge waliposhindwa kutetea ubingwa wao.

Hatua ya Conte kumsajili Mbelgiji, Michy Batshuayi kutoka Marseille na huku akihusishwa na mastraika wengine, ndicho kilichosababisha kuibuka kwa tetesi kuwa siku za Costa kwenye klabu hiyo zinahesabika.

Hata hivyo, Muitaliano huyo alimpa ujiko nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 wakati wa mechi za kujiandaa na msimu huu, akitaka kuona Costa akionyesha makali yake anapokuwa ndani ya eneo la hatari ili kuweza kuirejesha Chelsea kwenye medali ya juu ya soka la Uingereza.

“Diego ni straika na hilo nalifahamu, kwa mtazamo wangu mimi straika ndiye anayetakiwa kuwa roho ya timu,” alisema Conte.

“Sitaki straika kama huyo kuzunguukazunguuka tu uwanjani. Huwa napenda kuona anakaa ndani ya eneo la hatari kwa sababu yeye ni mshambuliaji na jukumu lake ni kufunga mabao na kuka katika nafasi mbadala. Wewe ni mshambuliaji, sio kiungo wala beki,” aliongeza Muitaliano huyo.


Alisema kuwa, kitu kingine ni kwamba huwa hapendi kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja lakini inategemea kutokana na kwamba Diego ni mchezaji mkubwa na mmaliziaji mzuri, lakini akasema kuwa pia anavyodhani bado anahitaji kuimarika zaidi.

No comments