ENGLAND, HISPANIA KUFUNGA MWAKA 2016 KWA KUCHEZA MECHI YA KIRAFIKI

TIMU za taifa za England na Hispania zinatarajia kufunga mwaka huu kwa kucheza mechi ya kirafiki ambayo itapigwa Novemba 15, kwenye uwanja wa Wembley.

Katika mwaka huu, mataifa yote hayo mawili yamefanya mabadiliko ya makocha ambapo kwa sasa England wako chini ya Sam Allardyce ambaye alikabidhiwa mikoba ya Roy Hodgson baada ya simba hao watatu kutolewa katika fainali za mataifa ya Ulaya “Euro 2016”, wakiwa hatua ya 16 Bora.

Huku Julen Lopetegui akichukua mikoba ya Hispania akimrithi Vicente del Bosque naye baada ya Hispania kuboronga katika hatua kama hiyo.

Hispania waliibuka washindi katika mechi iliyopita ambayo miamba hao walikutana Novemba mwaka jana mjini Alicente kwa ushindi wa mabao 2-1 yaliyowekwa kimiani na nyota wao Mario Gaspar na Santi Kazorla.

Kwa upande wa England, alikuwa ni kiungo mshambuliaji, Frank Lampard ambaye aliwahi kufunga bao pekee wakati timu hizo zilipokutana kwenye uwanja wa Wembley miaka mitano iliyopita.


Mtanange huo ndio utakuwa wa mwisho kwa miamba hao kukutana kwa mwaka huu, kutokana na kuwa zitafuatia mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia ambapo zote zitakuwa nyumbani kwa Scotland kuivaa England na Macedonia wakiwavaa Hispania.

No comments