GRANIT XHAKA AWAPA MASHABIKI WA ARSENAL NENO

MASHABIKI wa Arsenal itabidi wakenue meno tu kwani Granit Xhaka amekuwa katika ubora mkubwa tangu atue kikosini katika usajili wa msimu huu.

Kocha wa miamba hao wa Uingereza, Arsene Wenger ameanza kukisuka kikosi hicho akisema kwamba amechoka kulalamikiwa na wanazi wa klabu hiyo kutokana na kuishia nafasi za kawaida tu karibu kila msimu.

Arsene Wenger, kocha mzoefu katika Ligi Kuu ya Uingereza, aliamua kumsajili kiungo wa kati wa timu ya taifa ya Uswisi, Granit xhaka kutoka klabu ya Borussia Monchengladbach.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye amecheza kimataifa mara 41 na kuwa nahodha wa klabu hiyo ya Ujerumani, alijiunga na Arsenal kwa kiasi cha pauni mil 35 katika mkataba wa muda mrefu.

“Nafurahi kujiunga na Arsenal,” alisema Xhaka. “Nataka kuhamia mjini London ili kuiwakilisha klabu hii na kucheza katika Ligi ya Uingereza.”

“Nitafanya kila kitu kuwapatia taji Arsenal na kuwafurahisha mashabiki.”

Wenger alisema Granit Xhaka ni mchezaji mzuri aliye na uzoefu wa michuano ya klabu bingwa Ulaya na ile ya Bundesliga.

“Tumekuwa tukimfuatilia kwa muda mrefu na ni mchezaji atakayeongeza maarifa katika kikosi chetu.”

Wenger amesema kwamba anajua mashabiki wa Arsenal wana kiu ya kuona timu yao inapata mafanikio makubwa zaidi, lakini akasema huwezi kupata mafanikio hayo kama huna wachezaji wanaojitambua.


“Ukiwa na wachezaji wote wanaojua kazi yao, maana yake ni kwamba wewe kocha unayefundisha timu hiyo unapata urahisi wa kuamua cha kufanya,” amesema Wenger.

No comments