JOSE MOURINHO ASEMA POGBA ANA KAZI MAALUM OLD TRAFFORD

KOCHA mwenye maneno mengi ya shombo, Jose Mourinho amesema klabu ya Manchester United haijakurupuka kumsajili kiungo Paul Pogba.

Alisema alipanga kumrudisha mchezaji huyo Old Trafford kwa gharama yoyote kwasababu ana jukumu malum analotakiwa.

Mourinho ambaye ameanza kazi United kwa kuipa Ngao ya Jamii kwa kuichapa Leicester City katika mechi yake rasmi ya kwanza baada ya zile za kirafiki za maandalizi ya msimu mpya, amesema ametua kurudisha furaha ya mashabiki.

“Pogba amekuja wakati maalum kwa kazi maalum ya kufanya,” alisema bila kufafanua.

Alitamba kwamba yeye analijua soka la Uingereza, anawajua wachezaji na makocha wengi wa timu pinzani, hivyo hatarajii kutoka patupu katika msimu huu.

“Ikiwa unakwenda sehemu na unajua uendako kazi inakuwa rahisi sasa, naamini United iko tayari kutwaa ubingwa wa England msimu huu, japo ni mapema sana kwetu,” alisema Mourinho.

Alisema anaijua United kuliko wengine wanavyomdhania, anawajua wachezaji mmoja mmoja na anajiandaa kuwatumia wote ili kufanikisha kile kinachosubiriwa na mashabiki.

Mreno huyo akatamba kwamba hajamsajili mchezaji hata mmoja kwa ajili ya kufanya safari za kitalii bali ili watwae mataji.

Amewadhihaki makocha wa Arsenal, Arsene Wenger na mwenzake wa Liverpool, Jurgen Klopp kwamba wasitarajie watauweza moto wa United.

Pogba amerudishwa Old Trafford kwa takriban pauni mil 100 ambazo ni zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 280, akitokea Juventus, Italia.

No comments