KAKA AMVULIA KOFIA CRISTIANO RONALDO… asema ndiye anayestahili kuitwa mwanasoka bora wa dunia

SUPASTAA ambaye ni raia wa Brazil, Kaka amempigia saluti Cristiano Ronaldo na kusema kuwa kwa sasa ndiye mwanasoka wa kiwango cha juu anayestahili kuitwa mwanasoka bora wa Dunia.

Kaka aliyewahi kukipiga pia katika klabu ya Real Madrid anayoitumikia nyota huyo wa Ureno, alisema hayo na kunukuliwa na ESPN.

Mbrazil huyo mwenye umri wa miaka 34 kwa sasa anasakata soka la kimaslahi katika timu ya Orlando City ya nchini Marekani inayoshiriki Major League Soccer.

Akinukuliwa, Kaka alisema pamoja na kupita wanandinga mbalimbali kama Ronaldo de Lima na hata Lionel Messi, lakini Cristiano Ronaldo kwa sasa yuko juu.

“Cristiano ni mchezaji wa mfano usiowahi kutokea, hubadilika kila siku na kuwa katika kiwango kisichotarajiwa.”

“Kila msimu amekuwa anafanya jambo linalowashangaza wengi ikiwa ni pamoja na kutoshuka kiwango.”

“Ronaldo wa leo hawezi kuwa yule wa msimu uliopita, hubadilika kulingana na msimu na msimu, hasa kwa timu anazozitumikia.”

“Hata msimu huu ameweka rekodi ambayo awali hakuna mtu aliyetarajia. Amekuwa na mchango mkubwa kwa taifa la Ureno kutwaa uchampioni wa mataifa ya Ulaya,” alisema Kaka.

“Lakini hata alipoiwezesha Real Madrid kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, hakuna aliyemshangaa kwa sababu ni kati ya wachezaji wanaopambana siku zote.”

“Yupo pia Messi ambaye nae ni wa kiwango cha aina yake, lakini kwa sasa Ronaldo ni kama mfano wa mchezaji anayeweza kubadilisha matokeo wakati wowote.”


“Ameshinda mataji yote makubwa duniani akiwa na timu mbalimbali na sasa ni mchezaji wa mfano akiwa ndani ya Real Madrid.”

No comments