MARIA SHARAPOVA AELEKEA KUSHINDA KESI YA MATUMIZI YA DAWA ZISIZORUHUSIWA MICHEZONI... kurejea uwanjani Januari mwakani

RAIS wa chama cha mchezo wa tenisi nchini Russia, Shamil Tarpishchev amethibitisha kuwa kinara wa mchezo huo, Maria Sharapova atarejea uwanjani kuanzia Januari mwakani.

Bingwa huyo mara tano wa michuano ya Grand Slam alifungiwa kucheza miaka miwili na shirikisho la kimataifa la mchezo huo Machi mwaka huu, baada ya kubainika kutumia dawa zisizoruhusiwa michezoni wakati wa michuano ya wazi ya Australia ya mwaka huu.

Katika utetezi wake, bingwa huyo namba moja alidai kuwa alikuwa hafahamu kuhusu dawa hizo na huku akidai Taasisi ya kupambana na matumizi ya dawa iliongeza orodha hiyo mwanzoni mwa mwaka huu.

Baada ya kupewa adhabu hiyo, Sharapova alikata rufa kwenye mahakama ya usuluhishi wa masuala ya michezo, ambapo uamuzi wa kesi hiyo ungetolewa mwezi ujao lakini ukacheleweshwa kutokana na kukosekana na ushahidi wa kutosha.

Kutokana na hali hiyo, Tarpischev anaamini nyota huyo mwenye umri wa miaka 29, atashinda rufaa hiyo na atakuwa tayari kushiriki kwenye mashindano ya WTA Tour yanayotarajiwa kufanyika mapema mwakani.

“Uamuzi utafanyika septemba mwaka huu,” rais huyo aliliambia shirika la habari Russia, TASS.


“Sio kwamba nina uhakika wa moja kwa moja, lakini nina imani ataanza kucheza Januari 2017,” aliongeza rais huyo.  

No comments