SEBASTIEN SQUILLACI AITABIRIA UBINGWA ARSENAL HATA BILA KUSAJILI WAPYA

KWA lugha nyepesi unaweza kusema kuwa ni “jeuri”, utakapoitafakari kauli ya beki wa zamani wa Arsenal, Sebastien Squillaci, baada ya kusema kwamba bado wataleta ushindani katika mbio za kuwania ubingwa, hata wasiposajili wakati wa majira haya ya joto.

Nyota huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa ambaye aliitumikia klabu hiyo ya kaskazini mwa jiji la London kati ya msimu wa 2010 na 2013, kwa sasa anajianda na msimu mpya wa Ligi ya Ligue 1 akiwa na timu ya Bastia.

Akizungumza juzi, nyota huyo alisema kuwa anavyoamini kikosi hicho cha Arsene Wenger kina kila kitu cha kuwawezesha kufanya vizuri licha ya kuwepo na ujio wa wachezaji na makocha wengi wazuri.

“Msimu uliopita walikuwa ni Arsenal ambao walimaliza Ligi wakiwa nafasi ya pili na hivyo wana uzoefu mkubwa kwa miaka mingi,” alisema beki huyo katika mahojiano na mtandao wa Goal.

“Ni timu ambayo ina kikosi kizuri kila mwaka na hata kama hawatafanya usajili mwaka huu, nadhani Arsenal itakuwa ni timu ambayo italeta ushindani katika mbio za kuwania ubingwa, ” aliongeza staa huyo.


Alisema kwamba, wameshashuhudia ujio wa makocha wengi kwenye michuano ya Ligi Kuu England na wote wana uzoefu wa kutwaa ubingwa wakiwa na klabu kubwa na akasema kwamba anavyodhani itakuwa vita kubwa nzuri kutokana na ujio huo.

No comments