SVEN-GORAN ERIKSSON ATABIRI NEEMA KWA PEP GUARDIOLA

KOCHA wa zamani wa Manchester City, Sven-Goran Eriksson amesema kwamba hana wasiwasi kama Pep Guardiola atashindwa kupata mafanikio kwenye michuano ya Ligi Kuu England.

Guardiola amewasili jijini Manchester kwa matarajio makubwa kutokana na mataji ambayo ameyapata akiwa na timu vigogo Ulaya, Barcelona na Bayern Munich.

Katika kipindi cha miaka minne ambayo aliinoa Barca, mashabiki wao waliweza kufurahia mataji 14, matatu yalikuwa ni ya La Liga na mawili ni ya Ligi ya Mabingwa, huku akiiwezesha Bundesliga kutwaa mataji matatu mfululizo.

Kwa sasa Guardiola anajiandaa na mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu wakati Man City watakapokata utepe kwa kukutana na Sunderland wakiwa nyumbani hapo baadae leo.

Kutokana na hali hiyo, Eriksson ambaye aliiongoza Man City msimu mmoja wa 2007/08 ana uhakika raia huyo wa Hispania kuna makubwa atakayoyafanya akiwa na klabu hiyo ya jijini Manchester, huku akielezea kufahamu fika upinzani uliopo baina yake na kocha mpya wa Manchester United, Jose Mourinho.

“Guardiola atafanya vizuri akiwa na Man City kwenye michuano ya Ligi Kuu England, hakuna wasiwasi katika hilo,” Eriksson aliuambia mtandao wa Omnisport.

“Amewahi kushinda kila kitu nchini Hispania akafanya hivyo pia Ujerumani akiwa na Bayern Munich, hivyo nina uhakika atakwenda kufanya makubwa hapo.”


“Jambo hilo litakuwa vizuri kwenye Ligi Kuu na Man City ya Manchester. Timu moja itakuwa na Mourinho na huku nyingine ikiwa na Guardiola,” aliongeza kocha huyo wa zamani. 

No comments