ZLATAN IBRAHIMOVIC ATANGAZA KUONGEZA MKATABA MANCHESTER UNITED

KWA kile ambacho unaweza kusema ni kama kanogewa, straika Zlatan Ibrahimovic amesema kwamba anayafurahia maisha Manchester United na akasema kwamba ataogeza mkataba ili aweze kuendelea kuitumikia klabu hiyo ya Old Trafford.

Ibrahimovic aliwatema mabingwa wa Ufaransa Paris Saint-Germain Julai mwaka huu na kwenda kujiunga na Man United akiwa mchezaji huru na kupewa mkataba wa mwaka mmoja, lakini kukiwepo na uwezekano wa kuongeza mwingine mmoja.

Tangu awasili kwenye klabu hiyo, nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Sweden mwenye umri wa miaka 34, kwa haraka aliweza kuonyesha cheche zake kwa kufunga la kwanza wakati wa mechi za kirafiki kabla ya kufunga la ushindi wakati wa mechi ya kuwania Ngao la Jamii dhidi ya Leicester City.

Kutokana na mafanikio hayo ya haraka, Ibrahimovic kwa sasa amenogewa na kushindwa kupanga muda rasmi atakaoitumikia Man United wakati juzi akijiandaa kuivaa Bournemouth katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu England waliotoka na ushindi wa mabao 3-1.

“Ngoja tutaona kitakachojitokeza. Hauwezi kufahamu. Inaweza kuwa ni zaidi ya miaka miwili, ikawa zaidi ya mitatu. Ngoja labda tuone nitakavyocheza,” Ibahimovic aliliambia Sky Sport.


“Mimi siwezi kuwa mahali fulani kwa sababu ni Ibrahimovic. Natakiwa kuwa mahali kwa sababu ya kufanya vizuri na kuleta matokeo safi,” aliongeza staa huyo.

No comments