ALEXIS SANCHEZ AMTINGISHIA KIBERITI KOCHA WAKE ARSENE WENGER

MSHAMBULIAJI mahiri, Alexis Sanchez ameanza kumuonyesha kiburi kocha Arsene Wenger baada ya kumwambia amuongezee pauni 35,000 katika mshahara wake wa kila wiki.

Mkataba wa sasa wa Sanchez utamalizika mwaka 2018 na Wenger aliyevutiwa na kiwango cha mshambuliaji huyo alimuomba waanze majadiliano ya mkataba mpya.

Sanchez hakutaka kuzunguusha mambo, akamwambia amlipe pauni 175, 000 kwa wiki ikiwa kweli anataka aongeze mkataba, jambo ambalo ni kama kumtingisha Wenger.

Kwa sasa mshambuliaji huyo analipwa pauni 140,000 kwa wiki, akiwa kwenye kundi la mastaa wachache wanaolipwa fedha nyingi Emirates.
Mshambuliaji huyo juzi aliifungia Arsenal bao la kusawazisha katika mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa.

Katika mchezo huo, wenyeji PSG walijipatia bao la kuongoza katika sekunde ya 42 baada ya Edinson Cavani kutumia uzoefu kuwazunguuka walinzi wa Arsenal na kipa wao, David Ospina.


Tayari Sanchez ameshaifungia Arsenal mabao 43 katika jumla ya mechi 97 alizoichezea baada ya kutua Emirates mwaka 2014.

No comments