AYA 15 ZA SAID MDOE: HONGERENI DAR MUSICA ILA BADO SIJAWASOMA


MAJUZI Ijumaa ya Septemba 16 ilizinduliwa rasmi bendi ya Dar Musica pale Mango Garden Kinondoni na kuhudhuriwa na mashabiki wa kutosha.

Ilikuwa ni show inayoweza kumpa matumaini mwekezaji yeyote (Asiyejua madhila na gharama ya kuandaa tukio kama lile) kwa kuamini kuwa muziki wa dansi unalipa.

Dar Musica walipendeza sana kwa ‘pamba’ zao safi ambazo bila shaka zilimgharimu kiasi kikubwa cha fedha mmiliki wa bendi …ni bendi yenye uchu na ari ya kufanya makubwa kwenye muziki wa dansi, bendi iliyojaza wanamuziki wenye majina makubwa na uwezo wa hali ya juu.

Ilipigwa mipini flan ambayo ilidhihirisha kuwa Dar Musica ina wanamuziki wenye vidole vya biashara …nyuzi za magitaa zilinyanyaswa vizuri, tumba za Dulla Ngoma zilitamani kuongea kwa namna zilivyopata shurba, huku drums za Sele Kadance zikileta raha ya aina yake.

Yupo mtu mmoja anaitwa Fred Manzaka, mpiga kinanda ambaye nathubutu kusema ndiye anayeikuna zaidi roho yangu kuliko mpiga kinanda mwingine yeyote wa dansi hapa Bongo - huyu mtu nilianza kumwelewa siku nyingi sana tangu yuko Mashujaa Band, alinipa raha sana Ijumaa pale Mango Garden kwa namna alivyoushibisha muziki wa Dar Musica na kufanya kuwe na uwiano mzuri kati ya waimbaji na wapiga vyombo.

Rais wa bendi mwimbaji Jado Field Force hakoseagi pale linapokuja suala la kujiongeza na kujiamini, jamaa anajua ni namna gani mwanamuziki anatakiwa kujiongeza, namna gani awe na mwonekano mzuri jukwaani, big up Jado kwa eneo hilo ulitisha sana.

Raja Ladha, mwimbaji wa zamani wa Mashujaa Band naye ni miongoni mwa watu wanaounda safu kali ya waimbaji wa Dar Musica, lakini kuna mwimbaji mmoja aliyetambulishwa kwa jina la Eletee ndiye aliyenisisimua zaidi kwa namna alivyokuwa na njia tamu za uimbaji kupitia sauti yake tamu.


Pamoja na mengi mazuri yaliyojitokeza kuhusu Dar Musica, kuna mapungufu na kero ambazo hazipaswi kuachwa zipite hivi hivi bila kuzitanabaisha japo kwa uchache sana.

Katika kipindi hiki ambacho muziki kuendelea baada ya saa 6 za usiku ni ‘hisani’, Dar Musica hawakupaswa kuanza wimbo wao wa kwanza saa 7.23 za usiku, hawakaupaswa kuwa na porojo nyingi tangu saa 6 kamili baada ya bendi zilizosindikiza kumaliza ratiba yao.

Kwa takriban dakika 90 kabla ya wimbo wa kwanza wa Dar Musica, onyesho likapambwa na ‘siasa’ za hotuba, kutambulisha wakurugenzi wa bendi na maofisa wa kampuni iliyodhamini show, kutambulisha wanamuziki, ma –MC nao kupata wasaa wa kuonyesha uwezo wa kucheza, ili mradi kulikuwa na vitu vingi vilivyokula muda bila sababu za msingi.

Dar Musica imeondoka Mango Garden bila kutambulisha wimbo hata mmoja, yaani walifanya kama vile watu wote pale wanazijua nyimbo zao, wakatumbuiza kama vile wako mbele ya mashabiki wao wa kila siku ambao hawakuhitaji kujuzwa japo jina la wimbo na mtunzi, hili lilikuwa kosa la kiufundi kwani kunadi nyimbo lilikuwa jambo bora zaidi kuliko hata kutambulisha bendi.

Bendi hii si mpya, ina zaidi ya mwaka mmoja, ilianza na kina Edo Sanga na Karama Regessu lakini ikayeyuka  na hata ujio wa Jado na wenzake ulipelekea tukio la uzinduzi wa bendi ndani ya ukumbi wa Highway Night Park, Ukonga Jijini Dar miezi mingi iliyopita, hivyo onyesho la Mango Garden lingeleta maana zaidi kama lingekuwa ni la kutambulisha albam mpya na wasanii wapya na si uzinduzi wa bendi.

Kama Dar Musica wameandaa onyesho lile kuashiria kuwa sasa wanaachana na show za kiingilio kinywaji na kuanza rasmi kuchanja kiingilio cha pesa mlangoni, basi kidogo ninaweza nikashawishika kuwaelewa na nitawaomba siku moja warejee tena Mango Garden bila kusindikizwa na bendi yoyote ili tutathmini vizuri uwezo wao, kinyume na hapo nitazidi kusisitiza kuwa tukio halikusatahili kuwa la uzinduzi wa bendi.

Licha ya Dar Musica kuundwa na idadi kubwa ya wasanii (kitu ambacho ni mzigo kwenye gharama za uendeshaji wa bendi), lakini bado imeshindwa kuwa na wimbo tishio (hit song) …watu wengi tumeondoka Mango Garden bila kushika kipande hata cha mstari mmoja wa wimbo wowote wa Dar Musica.

Kutengeneza nyimbo ngumu na zilizojaa ufundi bado sio suluhisho, kinachotakiwa ni kutengeneza nyimbo zitakazo kuwa rafiki na masikio na vinywa vya mashabiki, hadithi fupi na inayoleweka, njia nyepesi za uimbaji na za mpangilio wa vyombo kwa sababu mwisho wa siku mshabiki anataka kuimba, anataka kupiga kinanda au gitaa kwa mdomo …akiyashindwa hayo basi ujue wimbo wako hauna nafasi kwake.

No comments