AYA 15 ZA SAID MDOE: SHOW ZA KIINGILIO KINYWAJI HAZIKWEPEKI


MUZIKI wa kiingilio kinywaji haukwepeki tena, hali ya uchumi imekuwa ngumu na bendi nyingi zinashindwa kufanya maonyesho ya kiingilio cha pesa.

Sasa hivi ni mwendo wa show za bure, mwenye ukumbi anamaliza kila kitu na kisha mwanamuziki ndiyo anakuwa muhubiri wa kuhimiza wateja waongeze salio mezani.

Zamani kulikuwa na bendi hazikubali kupiga bure hata uwape pesa mara mbili ya bei yao kawaida, kitendo cha kwenda kupiga kwenye bar kwa kiingilio cha kinywaji ilikuwa ni sumu kwao …labda ‘itokee’ tu.

Sasa hivi unaweza ukazitafuta kwa tochi bendi zinazokataa show za kiingilio kinywaji kwenye bar na kumbi za starehe …Ni mwendo wa kusuka au kunyoa – kataa show bure ukose cha kuwalipa wasanii wako au pokea show za bure ili angalau bendi ipumulie gesi.

Siku zote nimekuwa mpinzani mkubwa wa show za bure nikiamini kuwa zinaporomosha muziki wa dansi na taarab, lakini wakati mwingine unalazimika kuwahurumia wamiliki wa bendi kwa hasara kubwa wanazopota kutokana na show za kiingilio cha mlangoni.

Mapromota waliokuwa wakikodi hizi bendi na kupunguza mzigo wa uendeshaji kwa wamiliki wameyeyuka huku sababu kubwa ikiwa ni hasara wanazopata.

Kwamba kila promota anayekodi bendi na kuingia gharama kibao ikiwemo matangazo ya show na kulipia ukumbi, anajikuta akishindwa kurejesha gharama zake, mtaji unapungua siku hadi siku na hatimaye kukata shauri kuwa muziki haulipi tena.

Kutokana na hali hiyo, mzigo wa kuandaa show umerejea kwa wenye bendi, show inaandaliwa kwa gharama ya shilingi laki tano hadi saba, kisha show inaingiza shilingi milioni moja, ukitoa gharama za show unabakiwa na shilingi laki tatu, ukilipa posho za wasanii na gharama za usafiri huna unachobakiwa nacho na wakati mwingine unalazimika kuazima pesa kwenye akiba yako nyingine ili kufidia mapengo.

Na hapo ndipo show za bure zinapokuwa hazikwepeki …Mwenye bar anakupa laki sita ambayo haikugharimu chochote kuanzia matangazo hadi kulipia ukumbi.

Ukilinganisha shilingi laki sita na ile laki tatu uliyopata baada ya kutoa gharama za maandalizi ya show, unajikuta huna hatua nyingine ya kufanya zaidi ya kutia kibindoni laki sita na kupunguza mlolongo wa show zako za kiingilio cha mlangoni. Sio siri kuwa show za bure zinatia lawama na aibu lakini mwisho wa siku, unaambiwa heri lawama kuliko fedheha.

Nini kinatakiwa kufanywa na bendi zetu katika kipindi hiki cha mpito? Je zibweteke na show za bure? Hapana hata kidogo …Show za bure ni njia katika moja ya njia za bendi zetu kuelekea ‘kaburini’, ni show za kuogopa kama ukoma kwa sababu hiyo ndiyo hatua ya mwisho kabla bendi haijaitwa marehemu.

Jiulize ni hatua gani atakayochukua siku mwenye bar akiona hapati tena faida …iko wazi kabisa – atakushusha bei tena na tena, mwisho wa siku atakatisha mkataba. Yakikuta hayo katika bar zote tatu unazozitegemea bendi yako INAKUFA kwa kuwa huna tena uwezo wa kurudi kwenye show za kiingilio.

Bendi hazipaswi kubweteka, zinapaswa kuzichukua show za kiingilio kinywaji kama changamoto na kichocheo cha kujipanga upya, zipige kazi ya nguvu ili kuteka mashabiki wapya watakothubutu kulipa kiingilio siku ikibidi kufanya hivyo.

Bendi zisikubali kuwa na show zote za bure, zihakikishe zinakuwa na ngome moja au mbili kila wiki ambazo zitakuwa ni za kiingilio cha mlangoni hata ikibidi kukopa kutoka kwenye kile wanachovuna kwenye show zao za kiingilio kinywaji.

Kutokuwa na ujasiri wa kufanya japo onyesho moja la kiingilio kwa wiki, ni sawa na kujitanguliza chumba cha wagonjwa mahututi kabla hata hujawa mahututi.

No comments