Habari

AYA 15 ZA SAID MDOE: TWANGA PEPETA NA MASHAUZI CLASSIC MTAVUNA MLICHOPANDA

on

PENGINE katika kuashiria mipango mibovu ya maandalizi ya sikukuu kwa
bendi zetu au ile hali ya kukumbuka shuka alfajiri, ‘bendi’ za Twanga Pepeta na
Mashauzi Classic, zitafanya maonyesho yao ya Eid el Hajj pua na mdomo.
Leo Idd Mosi Mashauzi Classic watakuwa Mango Garden Kinondoni wakati
Twanga Pepeta watakuwa Vijana Social Hall Kinondoni – kumbi mbili zinazopakana.
Wakati Mashauzi Classic wakianza onyesho lao saa 3 usiku hadi usiku
mnene kwa kiingilio cha shilingi 7000, Twanga Pepeta wataanza onyesho lao saa
10 jioni hadi usiku mnene kwa kiingilio cha shilingi 5000.
Bendi zote hizo mbili (moja ya dansi na moja ya taarab) zinautumia
ukumbi wa Mango Garden kama ukumbi wao wa nyumbani.
Mashauzi Classic limekuwa likipiga hapo kila Alhamisi tangu kundi hilo
lianzishwe miaka mitano iliyopita huku Twanga wakipatikana Mango kila siku za
Jumamosi kwa zaidi ya miaka 15.
Lakini mara nyingi  makundi hayo
mawili pia yamekuwa yakipatikana Mango Garden wakati wa sikukuu kubwa kama
Pasaka, Idd na X-Mas kutegemea na nani amejipanga vipi.
Sipendi kusema nani kati yao amemfuata mwenzake, nani aliwahi
kutangaza ratiba yake ya sikukuu, wala sipendi kuweka dhana kuwa yupo aliyeamua
kumkomoa mwenzake, lakini ukweli ni kwamba licha ya kuwa bendi hizo zinapiga
aina tofauti ya muziki, ipo itakayoathirika kibiashara kama si zote.
Soko la muziki limekuwa gumu sana, pesa imekuwa ngumu hivyo bendi
mbili kutumbuiza katika kumbi zinazopakana, biashara lazima iwe ngumu – nimewahi
kujiridhisha na hilo pale FM Academia ilipokutana na Ogopa Kopa Kigamboni
kwenye kumbi zilizo jirani, Jahazi na Malaika walivyowahi kukutana Morogoro, Mashauzi
na Lady Jay Dee walivyoumana siku moja Morogoro, Christian Bella na King Kiki
ndani ya Dodoma – hiyo ikiwa ni mifano michache tu.
Nusu ya mashabiki wa eneo moja ndiyo wale wale wanaokwenda kwenye
kumbi za starehe bila kujali kama ni taarab au dansi, kwa hiyo kwa mazingira
waliyojiwekea Twanga na Mashauzi siku ya Idd, ni wazi kuwa yatawayumbisha
baadhi ya mashabiki.
Ni kweli kuwa Twanga Pepeta ina mashabiki wao wa damu na Mashauzi nayo
ina mashabiki wake wa damu, lakini wale mashabiki wasio na upande ndiyo
watakatoa hukumu ya mchuano huo usio rasmi.
Mwishoni mwa mwezi Julai yaliandaliwa matamasha mawili makubwa –
Tanzania Band Festival na Mwendokasi Festival – moja likifanyika Leaders Club
Kinondoni na lingine Chuo Posta Kijitonyama.
Matokeo ya matamasha hayo kufanyika kwa siku moja yalikuwa wazi – kila
moja lilipata hasara na bila shaka kila mwaandaaji aliyemfuata mwenzake
alijilaumu huku yule aliyefuatwa akisononeka.
Kwa ukaribu walionao wamiliki wa Twanga Pepeta na Mashauzi Classic, ni
wazi kuwa walistahili kuketi pamoja na kufanya tathmin ya faida na hasara ya
show zao kuwa jirani hasa kutokana na ukweli kuwa matukio kama hayo yamekuwa
yakipunguza upendo baina kundi moja na lingine.
Wamiliki bendi za dansi na taarab ni lazima wakubali kuwa soko
limeporomoka hivyo wanapaswa kupeana pumzi na kuachiana nafasi kwenye maonyesho
yao maalum hususan siku za sikukuu.
Wakati wamiliki hao wakilalamika kila kukicha kuwa muziki dansi na
taarab unamezwa na vyombo vya habari, wao wanapaswa kuwa mstari wa mbele
kuonyesha ubunifu wenye tija, upendo na mshikamano.

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *