CRISTHIAN STUANI AMPIGA BAO ZLATAN IBRAHIMOVIC

WAKATI mshambuliaji nyota wa Manchester United raia wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic akiendelea kung’ara katika Ligi Kuu ya England, bado nyota huyo hajafunga bao la kuvutia tangu Ligi Kuu ianze.

Taarifa ya chama cha soka cha Uingereza, imesema kwamba bao bora kabisa la mwezi Agosti limepachikwa na nyota wa Middlesbrough, Cristhian Stuani na kuwaacha Zlatan Ibrahimovic na Jamie Vardy wa Leicester City kwa mbili.

Cristhian Stuani amepata tuzo hiyo ya bao bora la mwezi katika mechi ambayo timu yake ya Middlesbrough ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sunderland.

Nyota huyo wa Uruguay alifunga bao ambalo lilikuwa kali kwa shuti la mbali katika dimba la Stadium of Light, ambalo limempa tuzo hiyo ambayo inatolewa kwa mujibu wa utaratibu wa FA ya Uingereza.

Lakini katika tuzo hiyo alikuwa anashindana na Zlatan Ibrahimovic ambaye bao lake lilitinga kwenye nyavu za Bournemouth, Philippe Coutinho wa Liverpool ambaye bao lake liliwachapa Arsenal na bao la Jamie Vardy dhidi ya Swansea City.  

Baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo, mchezaji huyo amesema kwamba anajisikia raha kuona ameanza vyema Ligi kwa mafanikio na ameahidi kupachika mabao mazuri zaidi.


“Tumekuwa tukishirikiana vyema na wenzangu na nimekuwa nikifunga mabao kama haya, lakini pia naahidi kufunga mabao makali zaidi,” amesema. Mchezaji huyo amesema kwamba anaamini kwamba bao hilo linaweza pia kuwa bao la msimu kama hatafunga bao kali zaidi ya hilo.

No comments