EDEN HAZARD AMBEZA MOURINHO KUPITIA CONTE... asema Conte anafahamu jinsi ya kuishi na wachezaji

STAA wa Chelsea Eden Hazard anaonekana kuanza kumchimba kocha wake wa zamani, Jose Mourinho baada ya kumpongeza Antonio Conte kwa jinsi anavyoishi vizuri na wachezaji wake.

Kibarua cha Mourinho kwenye klabu hiyo ya Stamford Bridge kilifikia ukomo kabla ya Sikukuu ya Krismasi mwaka jana, baada ya timu yake kupoteza mechi tisa kati ya 16 za kwanza msimu huo.

Katika kipindi hicho uhusiano wa Mreno huyo na wachezaji nyota akiwemo Hazard ulikuwa sio mzuri mno.
Msimu huu kiwango cha Hazard kilionekana kushuka lakini chini ya Conte kwa sasa anaonekana kuwa moto wa kuotea mbali baada ya kufunga mabao mawili katika mechi tatu za kwanza msimu huu.

Akizungumza jana na gazeti la ‘Equipe, Hazard alisema kuwa Conte amekuwa akimwania kila mchezaji na kwamba sasa wapo vizuri baada ya mwaka jana kuvurunda.

“Conte amekuwa akimwamini kila mchezaji na sasa tupo vizuri baada ya msimu uliopita kufanya vibaya,” alisema nyota huyo.

“Mara zote tupo wachezaji walewale lakini Conte anafahamu jinsi ya kuishi na wachezaji na ndio maana tunacheza kwa kiwango cha hali ya juu,” aliongeza staa huyo.

No comments