FELLA ALIPOAMUA KUZIWEKA HADHARANI NYUMBA WALIZOJENGEWA WASANII WA YAMOTO BAND


MKURUGENZI wa kituo cha Mkubwa na Wanawe, Said Fella jana alizifichua rasmi nyumba takribani tano za wasanii wake wa kundi la Yamoto Band na kuwataka wananchi waelewe kuwa msanii anahitaji nyumba na sio magari.

Nyumba hizo zilizojengwa nje ya mji kidogo, katika kata ya Kisewe amesema kuwa hiyo ni moja ya maendeleo kwa wasanii kwani hii si mara ya kwanza kuwazawadia nyumba wasanii wake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam, Fella amesema kuwa ameamua kuziweka wazi hasa baada ya kusikia maneno mengi kutoka kwa wananchi wakidai kuwa Yamoto Band hawafaidiki na muziki wanaoufanya.

Fella amesema kuwa nyumba hizo mpaka sasa hajajua thamani yake ila zitakapokamilika ataita watu wa tathmini kwa ajili ya kuziangalia ili kujua zimetumika kiasi gani kwenye ujenzi huo.

Ametoa shukrani za dhati kwa Raisi wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete kwa juhudi kubwa sana alizozifanya katika kuhakikisha anafanikiwa kuinua wasanii.

Nyumba hizo zitakazozinduliwa hivi karibuni ni maalum kwaajili ya wasanii vinara wa Yamoto Band – Aslay, Enock Bella, Maromboso na Beka One.

Lakini ipo pia nyumba kwaajili ya mshindi wa BSS 2015 Kayumba Juma ambaye naye ni mwanafamilia wa Mkubwa na Wanawe.

Meneja wa Mkubwa na Wanawe, Amani Temba (Mh. Temba) amesema kuwa hizi nyumba zimejengwa kwa fedha za wasanii wenyewe wanazozipata kwenye shoo za muziki wanazozifanya na sio kama zimetoka mfukoni mwa kiongozi yoyote.

Mkurugenzi wa Twanga Pepeta Asha Baraka ambaye alikuwa mmoja wa waalikwa wa tukio hilo, akasema amefurahishwa na hatua hiyo kwani ni mara chache sana kwa viongozi wa muziki kuchukua dhamana ya kuwajengea nyumba wasanii wao.
  Said Fella (kushoto) akifafanua jambo
 Mkurugenzi wa Twanga Pepeta Asha Baraka akipongeza hatua ya Fella
Safu ya nyumba za wasanii wa Yamoto Band


No comments