GARETH BALE ATAKA AZIDISHIWE DAU NDIPO ASAINI MKATABA MPYA

GARETH Bale ni kama anatikisa kiberiti ama tuseme sikio limezidi kiichwa. Nyota huyo wa Wales amesema kwamba hawezi kusaini mkataba mwingine kwa bei ileile.

Mchezaji huyo ambaye alisajiliwa na Real Madrid kwa zaidi ya pauni mil 80 amesema kwamba hatasaini mkataba mpya mpaka pale timu hiyo litakapoweka dau linalozidi kiwango cha Neymar.

Real Madrid iko katika mazungumzo na Bale kwa ajili ya kusaini mkataba mpya baada ya mkataba wake wa awali wa miaka mitano kukaribia kukatika, lakini amesema kwamba hatasaini mkataba wa “kitoto”.

Nyota huyo ameshapachika mabao 19 katika michezo 23 aliyocheza msimu uliopita, sasa anapokea mshahara wa euro 180,000 kwa wiki katika kikosi hicho cha Real Madrid.
Amesema kwamba yeye ni muhimu katika kikosi hicho na anataka kuona kwamba analipwa mshahara unaofanana na ule ambao Neymar analipwa na FC Barcelona tena baada ya timu ya Paris Saint-Germain kuonyesha nia ya kumtaka raia huyo wa Brazil.


Wakati ambao Madrid wamezuiwa na FIFA kufanya usajili kwa misimu miwili, wanalazimika pia kurekebisha mikataba ya wachezaji wake, Cristiano Ronaldo, Luka Modric na Toni Kroos, lakini Bale yuko katika malengo ya rais wa Real Madrid, Florentino Perez kwamba abaki hapo hadi mwaka 2021.

No comments