JAMIE VARDY AANIKA SABABU ILIYOMFANYA KUITOSA ARSENAL

MFUMANIA nyavu wa Leicester City, Jamie Vardy ameweka wazi sababu ya kwanini alikataa ofa ya kujiunga na Arsenal katika usajili wa msimu uliopita.

Akibainisha, straika huyo alisema alifanya hivyo kwa kuzingatia mustakabali wa soka lake na klabu anayoitumikia hivi sasa.

Kisha akasema alitumia akili na utashi mkubwa kufikia uamuzi wa kubakia katika kikosi cha mbweha hao wa jiji la Leicester City.

Vardy alitajwa katika usajili wa awali wa klabu ya Arsenal uliokuwa na ofa ya pauni mil 20, kabla ya siku chache baadae kukanusha taarifa za usajili wake.

Akinukuliwa Vardy mwenye umri wa miaka 29, alisema ilimchukua masaa mengi ya kujifungia akiwa peke yake na kufikia uamuzi wa kukataa ofa ya The Gunners.

“Nilikuwa katika chumba cha hoteli kwa masaa mengi nikiwa sina la kufanya zaidi ya kuwaza nini cha kuamua dhidi ya Arsenal.”

“Sikutaka kuficha ukweli wa kile nilichoamua lakini ni kwamba uamuzi wa kuachana na ofa ulifikiwa kutoka kichwani na ndani ya moyo wangu kabla ya kufikia uamuzi sahihi.”

“Ulikuwa ni uamuzi mgumu katika kipindi cha maisha yangu ya soka, lakini ni uamuzi uliotokana na akili na moyo wangu bila kumshirikisha mtu mwingine,” alinukuliwa Vardy.


Vardy ambaye ni sehemu ya nyota wanaounda timu ya taifa ya England, hakupangwa katika kikosi cha kocha Sam Allardyce kilichoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Slovakia.

No comments