JUVENTUS WASEMA HAWAKUTAKA KUMUUZA POGBA MAN UNITED BALI ALING'ANG'ANIA

MKURUGENZI  mkuu wa mtendaji wa Juventus, Giuseppe Marotta amesema kwamba mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Italia serie A hawakutaka kumuuza nyota wao Paul Pogba, lakini kiungo huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa aliomba mwenyewe kuondoka.

Pogba mwenye umri wa miaka 23 aliondoka Juventus na kurejea Manchester United mwezi uliopita kwa ada ambayo ilivunja rekodi ya usajili duniani.

Fedha hizo alizonunuliwa Pogba ziliisaidia Juve kumnasa staa mwingine Gonzalo Higuain na wakati klabu hiyo ikifurahi kupata fungu hilo, Marotta anasema kwamba hawakutaka kumnunua Mfaransa huyo.

“Mara zote tulikuwa tukisema hatutaki kumuuza Pogba, alikuwa ni mchezaji muhimu kwa klabu kwa mashabiki na kocha,” alisema Marotta katika mahojiano na kituo cha televisheni cha JTV.

“Alitaka kubadili mazingira na kupata uzoefu tofauti na hivyo ndivyo maana tukaingia katika majadiliano ili kuweza kumfanya awe na furaha,” aliongeza mkurugenzi huyo.


Alisema kwamba tangu awali walikuwa wakimfuatilia Higuain kutokana na kuwa ndio sura iliyokuwa akilini mwao, lakini wakajikiuta wakifanikiwa kumnasa katika kipindi ambacho Pogba alikuwa ameomba kuondoka.

No comments