KOCHA BARCELONA AJIBEBESHA LAWAMA KIPIGO DHIDI YA DEPORTIVO ALAVES

KOCHA Luis Enrique amesema kwamba yeye ndiye anayepaswa kubeba lawama kutokana na kipigo cha kushitukiza cha mabao 2-1 ilichokipata Barcelona dhidi ya timu iliyopanda daraja msimu huu Deportivo Alaves wakiwa kwenye uwanja wao, Camp Nou juzi.

Katika mchezo huo, kocha huyo aliwaweka benchi nyota wake Lionel Messi na Luis Suarez kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Celtic na huku akimpanga Neymar ambaye amerejea hivi karibuni baada ya kumaliza michuano ya Olimpiki.

Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa Mbrazil huyo haikuweza kubadili matokeo ambapo ilishuhudiwa Alves wakiwa mbele mara mbili kupitia kwa nyota wao Deyverson na Ibai Gomez.

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo, Luis Enrique alieleza kufurahishwa na mbinu aliyoitumia kocha mwenzake Mauricio Pellegrino akisema kuwa hakutarajia kukutana na hali hiyo.

“Sote tulikuwa na matarajio ya kupata ushindi lakini wakatukumbusha jinsi kazi ilivyokuwa ngumu kufanya hivyo,” alisema kocha huyo.


“Lakini pamoja na hilo, kwangu mimi naweza kusema kuwa nastahili kubeba lawama kwa kipigo hiki,” aliongeza.

No comments