KUNGO KOKE WA ATLETICO MADRID ASEMA KIKOSI CHAO KIKO FITI KUWAVAA BARCELONA KESHOKUTWA

KIUNGO wa timu ya Atletico Madrid, Koke ni kama kaitishia nyau Barcelona baada ya kusema kuwa kikosi chao kiko katika ubora wa hali ya juu kuwakabili mahasimu wao hao katika mechi ya Ligi Kuu ya Hispania La Liga itakayopigwa keshokutwa.

Ushindi wa mabao 5-0 ambao waliupata juzi dhidi ya Sporting Gijon umekifanya kikosi hicho cha kocha Diego Simeone kushinda mechi tatu mfululizo bila kuruhusu bao na kunaifanya Atletico kubaki nyuma kwa pointi moja dhidi ya Barca ambayo nayo iliisambaratisha Leganes kwa mabao 5-1 kabla ya miamba hao kukutana kwenye uwanja wa Camp Nou.

Kutokana na hali hiyo, Koke ameelezea jinsi walivyojipanga kwa sasa baada ya kutoka sare mbili katika mechi zao za kwanza msimu huu kabla ya kuwavaa mabingwa hao wa Ligi hiyo.

“Hali hii ni lazima iendelee kuwa hivyo na tumeshanza na sasa tunakutana na Barcelona,” Koke aliliambia gazeti la Marca.

“Tunahitaji maombi kutoka dunia nzima ili tuweze kuondoka na pointi zote tatu licha ya kuwa ni mechi ngumu dhidi ya timu nzuri duniani lakini tuna matumaini, tutapambana na kuondoka na ushindi,” aliongeza nyota huyo.


Alisema kuwa wiki iliyopita ilikuwa nzuri kwao baada ya kupata ushindi mara tatu kutokana na kuwa kiwango chao kimekuwa kikiongezeka kila mechi na akasema kuwa kwa sasa wameshajiandaa kwa kila kitu.

No comments