MAKAMU WA RAIS BARCELONA ATIA NENO KUHUSU ADHABU YA REAL, ATLETICO MADRID KUPINGWA KWA KISHINDO

MAKAMU wa rais wa klabu ya Barcelona, Carles Vilarrubi amesema kwamba anashangaa kuona jinsi watu wanavyounga mkono kupinga adhabu ya kufungiwa kutosajili waliyopewa Real na Atletico Madrid akisema kwamba aliwahi kupiga kelele nyingi wakati timu yao hiyo ya Catalans ilipopewa adhabu kama hiyo miaka miwili iliyopita lakini hakuna aliyemuunga mkono.

Kauli ya kigogo huyo imekuja baada ya juzi Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA), kukataa rufaa zilizowasilishwa na klabu hizo mbili za Real na Atletico kupinga kufungiwa usajili misimu miwili kwa kuvunja kanuni za usajili wa kimataifa baada ya kutiwa hatiani kwa kusajili wachezaji wenye umri chini ya miaka 18, kama ilivyokuwa kwa Barcelona mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wengi wa soka nchini Hispania walisema adhabu zilizopewa klabu hizo mbili za jiji kuu la nchi hiyo haikustahili, lakini Vilarrub anasema kwamba Barcelona haikuungwa mkono kama hivyo.

“Miaka miwili iliyopita hatukuungwa mkono wowote, taifa lilikaa kimya kuhusu ukweli, kuna kampeni za ajabu dhidi yetu,” kigogo huyo wa Barcelona alikiambia kituo cha radio RAC1.


“Tulishutumiwa kwa kuwasafirisha watoto na shutuma nyingine chafu. Hivyo vyombo vya habari nchini ni lazima viwe makini kuheshimu kile kinachokiandika,” aliongeza rais huyo.

No comments