NEMANJA MATIC AFICHUA KUTOMHOFIA N'GOLO KANTE KATIKA VITA YA NAMBA CHELSEA

STAA wa Chelsea Nemanja Matic amesema kwamba kwa sasa hana wasiwasi kuhusu hatima ya kibarua chake katika klabu hiyo kutokana na ujio wa kiungo mpya, N’Golo Kante ambaye amesajiliwa msimu huu kutoka katika timu ya Leicester City.

Kinara huyo raia wa Serbia ni miongoni mwa wachezaji waliotoa mchango mkubwa kwa klabu hiyo hadi kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2014/15, lakini msimu uliopita akajikuta akifanya vibaya na kwa sasa alikuwa akionekana nafasi yake ipo shakani baada ya kuwasili Kante.

Hata hivyo, pamoja na hali hiyo Matic kwa sasa anasema kuwa hafikirii kuondoka Chelsea licha ya awali kuwepo na tetesi zilizokuwa zikidai kwamba huenda akaenda kujiunga na timu za Juventus na Manchester United kabla ya kuamua kubaki chini ya kocha mpya wa timu hiyo, Antonio Conte na huku akianzishwa kila mechi msimu huu.

“Kwa kuwa mkweli nimeshazungumza na Conte,” staa huyo aliliambia shirika la habari la Sky Sport.

“Nilizungumza na klabu na pande zote mbili zilisema kuwa ni jambo jema kwa klabu na mimi.”

“Nafurahi kwa sababu kwa sasa nipo na timu hii, nitajitolea kwa kila kitu na kwa kila uwezo wangu ili kuhakikisha timu inapigania ubingwa,” aliongeza staa huyo.


Alisema kwamba mara zote amekuwa akijisikia mwenye furaha kuwa kwenye timu hiyo na akasema kuwa anachokitaka ni kuboresha soka lake na huku akimpamba kocha wake, Conte.

No comments