PEPE ATAMANI KUZEEKEA REAL MADRID

STAA wa Real Madrid Pepe amesema ana mpango wa kumalizia maisha yake ya soka akiwa na miamba hiyo ya Bernabeu.

Mlinzi huyo wa kati raia wa Ureno ana miaka 33 na mkataba wake na Madrid utafikia tamati mwishoni mwa msimu huu.

Kwa upande wao, Madrid wameonyesha nia ya kuendelea na huduma ya beki huyo kisiki ambaye alikuwa na timu ya taifa ya Ureno iliyotwaa taji la michuano ya Euro 2016.

Imeelezwa kuwa mkali huyo anatarajiwa kupewa mkataba wa miaka miwili kuendelea kukipiga klabuni hapo.

“Niko huru hapa Real Madrid. Nina mkataba na nitasubiri mpaka dakika ya mwisho hapa. Bado kuna muda, umebaki mwaka mmoja,” alisema Pepe akiuambia mtandao wa Cadena SER.

“Ndio, ningependa kustaafu nikiwa hapa ingawa nina ofa kutoka katika klabu nyingine. Niliwambia wawakilishi wangu kuwa nataka kubaki hapa.”


Pepe ambaye alitua Madrid akitokea Porto mwaka 2007, ameichezea timu hiyo michezo 317, ameshinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na mawili ya La Liga.

No comments