PETER SCHMEICHEL ASEMA GUARDIOLA ALIIFANYA BAYERN MUNICH KUWA TIMU MBAYA

MLINDA mlango wa zamani Peter Schmeichel amemvaa kocha Pep Guardiola akisema kwamba aliifanya Bayern Munich kuwa timu mbaya kiasi cha kutoiangalia na huku akisema kwamba alikuwa na bahati kwa mafanikio aliyoyapata akiwa Barcelona kutokana na kwamba alikuwa na wachezaji wenye vipaji.

Katika kipindi cha miaka minne alichokaa kwenye klabu hiyo ya Camp Nou, kocha huyo wa Manchester City, Guardiola alifanikiwa kutwaa mataji matatu ya Ligi, ubingwa wa Cope del Rey na mara mbili akifanikiwa kutwaa wa Ligi ya mabingwa.

Baada ya kupata mafanikio hayo akiwa na klabu hiyo ya Catalan, kocha huyo aliendelea kufanya hivyo pia kwenye michuano ya Ligi ya Bundesliga akiwa na Bayern ambapo waliweza kutwaa mataji matatu ya Ligi kati ya mwaka 2014 na 2016 pamoja na lile la DFB-Pokal mara mbili.

Hata hivyo, pamoja na Guardiola ambaye alikabidhiwa timu kutoka kwa Jupp Heynckes kupata mafanikio hayo, Schmeichel anavyodhani Bayern ilikuwa ikitandaza kandanda safi wakati ilipokuwa chini ya Mjerumani tofauti na mbinu alizokuwa akitumia Guardiola.
“Alikuwa vizuri wakati akiwa Bayern Munich. Naweza kusema hivyo,” staa huyo aliuambia mtandao wa Omnisport.

“Lakini kwangu mimi binafsi naweza kusema timu ilibadilika na kuacha kucheza soka la kuvutia na badala yake ikawa imecheza soka ambalo huwezi kutamani kuliangalia,” aliongeza staa huyo wa zamani.

Schmeichel ambaye alicheza mechi 398 akiwa Manchester United, vilevile alisema kuwa anavyoamini mafanikio aliyoyapata Guardiola akiwa Barcelona yalitokana na kuwa alikuwa na wachezaji wakali kama vile Lionel Messi, Xavi na Andres Iniesta.


Mlinda mlango huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Denmark alidai pia itakuwa vigumu kwa kocha huyo kupata mafanikio kama hayo akiwa na Manchester City.

No comments