USAJILI WA PEP GUARDIOLA WAMKUNA KEVIN DE BRUYNE MANCHESTER CITY

KWA kile ambacho unaweza kusema ni kama usajili wa Manchester City umemkuna staa wao, Kevin De Bruyne, nyota huyo amesema kuwa wachezaji waliosajiliwa na kocha wao Pep Guardiola wamekiunganisha kikosi chao na kukifanya kipate kile ilichokuwa ikikihitaji.

De Bruyne alitakata katika msimu wake wa kwanza alipotua Etihad baada ya kufunga mabao na kutoa pasi zilizozaa mengine 14 kwa washindi hao wa Kombe la Ligi, lakini Man City wakajikuta wakishika nafasi ya nne katika michuano ya Ligi Kuu na huku aliyekuwa kocha wao, Manuel Pellegrini akiondolewa.

Juzi Man City waliinyuka Manchester United ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani, Old Trafford na huku mahasimu wao hao wakiwa wameshaanza dhana mpya chini ya kocha wao, Jose Mourinho ambaye alishawaonjesha ushindi kila mechi yao ya Ligi.

Katika mchezo huo ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0, Guardiola alimkosa mpachikaji mabao wake muhimu, Sergio Aguero lakini aliweza kumtumia nyota wa timu ya taifa ya Ujerumani, Leroy Sane na nyota wake mwingine, Nolito ambaye tayari alishaandika kwenye jina lake mabao matatu pamoja na mchezaji bora wa mwezi wa klabu hiyo, Raheem Sterling aliyeingia akitokea benchi.

“Mwaka jana nilikuwa nikijihisi mchanga ndani ya timu kwa sababu nilitoka mahali ambapo sikuwa na uzoefu mkubwa, licha ya kuwa nilikuwa na umri wa miaka 24, lakini kwa sasa kuna kizazi kipya ambacho kimekuja na nimepiga hatua ya pili katika kibarua changu,” nyota huyo wa timu ya taifa ya Ubelgiji aliwaambia waandishi wa habari.


“Vijana ambao wamekuja wana uwezo mkubwa wa kutoa pasi, wapo kama umeme. Ninavyodhani tumepata kitu ambacho mwaka jana tulikuwa tukikihitaji,” aliongeza nyota huyo.

No comments