XABI ALONSO AMTABIRIA MAKUBWA RENATO SANCHES BAYERN MUNICH

STAA Xabi Alonso ni kama kamtabiria makubwa nyota mwenzake, Renato Sanches, baada ya kusema kuwa yupo tayari kuisaidia Bayern Munich kutwaa ubingwa licha ya kuwa na umri mdogo.

Sanches aliondoka Benfica na kwenda kujiunga na Beyern msimu uliopita na kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 leo anatarajia kucheza mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Bundesliga dhidi ya Schalke.

Wakati mashabiki wakijiandaa kuona makali ya Mreno huyo ambaye ameshatwaa ubingwa wa fainali za Mataifa ya Ulaya “Euro 2016”, Alonso amekuwa wa kwanza kumpongeza kinda huyo.
“Atakuwa mchezaji tegemeo. Ana uwezo mkubwa, nguvu na ana hasira za kutwaa ubingwa. Chaguo zuri kwa klabu,” alisema Mhispania huyo.

“Umri sio tatizo. Ana miaka 19, lakini tayari ameshakuwa mchezaji mkubwa,” aliongeza staa huyo.

Alisema kuwa jambo hilo ndilo muhimu kwa kila mchezaji hata akiwa na umri 19 ama 35.

Sanches hajakanyaga uwanjani tangu alipoumia misuli ya nyama za paja mwezi uliopita, jambo ambalo lilimfanya akose mechi ya kwanza ambayo Bayern waliibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Werder Bremen. 

No comments