ARSENAL YATENGA DAU NONO KWA AJILI YA PIRRE-EMERICK AUBAMEYANG WA DORTMUND

KUFURU ya pesa inaendelea kuonyeshwa kwa klabu kubwa duniani ambapo sasa Arsenal imedaiwa kwamba imeshatenga kiasi kikubwa cha pesa kuinasa saini ya nyota wa Borussia Dortmund, Pirre-Emerick Aubameyang.

Habari zilizopatikana juzi kutoka mitandao ya kimataifa zinasema kwamba arsenal imepania kumalizana na mchezaji huyo raia wa Garbon katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo mwezi Januari kwa kitita cha pauni mil 52.

Arsenal ilitumia kiasi cha pauni mil 17 msimu huu kumsajili mshambuliaji wa klabu ya Deportivo La Coruna, Lucas Perez kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili msimu huu.

Kocha wa washika bunduki hao, Arsene Wenger alihamishia akili yake kwa Perez baada ya kushindwa kumsajili mshambuliaji wa Leicester, Jamie Vardy lakini pia nyota wa Lyon ya Ufaransa Alexandre Lacazette.

Sasa akili ya wenger ni kwa nyota huyo wa kimataifa wa Garbon ambaye amekuwa kwenye kiwango cha juu sana kwenye timu yake ya sasa nchini Ujerumani.

“Pierre-Emerick Aubameyang yuko kwenye kiwango cha juu kabisa na haitakuwa ajabu kumsajili. Unaweza kufananisha uwezo wake na wakati ule tulipomsajili Nwanko Kanu wa Nigeria au Emmanuel Adebayor wa Togo,” amesema Wenger akikaririwa na mtandao wa Express Sports.

Lakini mtandao mwingine wa El Confidencial umedai kwamba inawezekana kabisa aubameyang akahamia Arsenal mwezi Januari lakini si kwa kiwango ambacho kinatajwa.

Dortmund wanadaiwa kwamba wamekata ofa hiyo na wanataka walipwe euro mil 100 sawa na pauni mil 86.7 kama kweli Arsenal wanaitaka huduma ya nyota huyo.

El Confidencial imesema kwamba klabu nyingine ambazo zimeingia katika vita ya kumwania nyota huyo ni pamoja na Real Madrid na Bayern Munich ambazo zimeonyesha nia ya kumnasa nyota huyo.


Vita ya kumwania nyota huyo imewafanya pia mashabiki wa Chelsea kuanza kumwania mchezaji huyo wakati klabu nyinginbe za Atletico Madrid na Paris Saint-Germain zikitajwa kwamba zinahitaji huduma ya nyota huyo.

No comments