FILIPPE COUTINHO ASEMA KLOPP ANAIRUDISHA LIVERPOOL KWENYE UBORA WAKE

FILIPPE Coutinho wa Liverpool mwenye umri wa miaka 23, amenukuliwa akisema kuhusu Klopp kuwa tangu achukue jukumu la kuinoa Liverpool ameifanya timu kurudi taratibu kwenye mstari, japokuwa kuna changamoto nyingi za kukaa kileleni.

“Ukiniuliza mimi ninaweza kukwambia jambo moja kuwa Klopp ni kocha bora kwa sababu ameibadili timu tangu pale alipopewa jukumu.”

“Liverpool ya sasa ni tofauti na ile iliyokuwa chini ya Brendan Rodgers, kuna tofauti kubwa hata ya namna timu inavyocheza kwa wachezaji kushirikiana dimbani.”

“Tangu atue Anfield mwezi Oktoba, mwaka jana ameonyesha mambo mapya ambayo sisi kama wachezaji tunaweza tukawa sehemu ya kuzungumzia mabadiliko haya,” alisisitiza mwanandinga huyo raia wa Brazil.

“Tunacheza tukiwa na furaha na imani kubwa chini ya Klopp, kama atapewa muda zaidi wa kuendelea kuwa hapa nina imani kuwa kuna jambo inaweza kubadilika na hata timu kurejea katika kiwango cha soka la zamani.”

“Tupo katika mwendo wa mafanikio. Tunarudi katika mstari wetu wa siku nyingi nyuma ambapo soka letu lilikuwa katika kiwango chetu cha kawaida.”

“Ni kipindi ambacho hata mashabiki wetu lazima watambue kuwa tunapita katika kipindi cha mapito, lakini katika kipindi kifupi baadae Liverpool itabadilika na kuwa timu ya ushindani kama zamani.”


“Tukiwa mazoezini utaona jinsi tunavyowajibika huku tukifurahia mbinu zake mpya ambazo zinatufanya tuwe katika kiwango bora. Klopp ni kocha anayeangalia mbele kwa mtazamo wa mafanikio ya baadae,” alisisitiza Coutinho.

No comments