GUNDOGAN AAMINI PEP GUARDIOLA ATAISAIDIA MANCHESTER CITY KUIPIGA BARCELONA LEO

ILKAY Gundogan anaamini kwamba uzoefu mkubwa alionao Pep Guardiola kwa klabu ya Barcelona unaweza kuisaidia Manchester City kumnyamazisha Lionel Messi na kuchukua pointi zote tatu Camp Nou.

Guardiola anarejea Barca kwa mara ya pili akiwa kocha wakati anapoiongoza timu yake ya Man City katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya leo.

Alitwaa makombe 14 katika miaka minne aliyoifundisha Barca kati ya mwaka 2008 na 2012 na ndiye anayetajwa kuwa sababu kubwa ya kuinuka kwa Messi katika soka la dunia.

Guardiola alifungwa aliporejea Camp Nou kwa mara ya kwanza pale timu yake ya Bayern Munich ilipolala 3-0 katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2015 ambapo Messi alifunga magoli mawili na kupika jingine moja.

Lakini Gundogan anaamini kwamba City watabebwa na ufahamu alionao Pep katika klabu hiyo aliyejenga jina lake kama mchezaji na pia kocha.

“Ni faida kubwa kwetu kwa sababu anawafahamu,” mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani aliwaambia waandishi wa habari.

“Anaifahamu timu, klabu, uwanja na anamfahamu Messi.”
“Anaifahamu pia staili ya Barcelona, staili ya Catalunya, anajua kila kitu na atatupa baadhi ya dondoo ambazo kocha mwingine hawezi kutupa.”

“Hii ni muhimu, hakika. Anajua wanachezaje na vipi watataka kucheza. Mwishowe hata hivyo ni juu yetu wachezaji kuyatimiza uwanjani na kutimiza tunachotakiwa kufanya.”

Guardiola ameweka lengo la kupata pointi sita kutoka katika mechi zao nne za hatua ya makundi zilizobaki kufuatia sare ya 3-3 dhidi ya Celtic katika mechi iliyopita na anataka kuwafunga Barca kwenye uwanja wao wenyewe.


Gundogan anakubali kwamba huu ndio mtihani mkubwa zaidi kwa City kufikia sasa lakini amesisitiza kwamba wachezaji wenzake wamepandwa na mizuka badala ya kuhofia.

No comments