KOCHA MAURO BIELO ABAINISHA KILICHOMFANYA DROGBA AKATAE KUCHEZEA TIMU YAKE YA MONTREAL IMPACT

KOCHA wa timu ya Montreal Impact, Mauro Bielo amesema kuwa aliyekuwa mchezaji wa Chelsea, Didier Drogba alikataa kuichezea timu yake baada ya kuambiwa hataanzishwa kwenye kikosi cha kwanza wakati wa mchezo dhidi ya Toronto uliopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Drogba mwenye umri wa miaka 38, hakuwepo katika uwanja wa Saputo ambapo Impact ilipata sare ya 2-2 na hivyo basi kuweza kufuzu kwa michuano ya mtoano ya Marekani.

Montreal hapo awali ilikuwa imesema kuwa Drogba alikuwa anauguza jeraha la mgongo na hivyo basi asingeweza kucheza.

“Hakukubali kwamba angeshezeshwa kama mchezaji wa ziada na mwishowe hakutaka kushirikishwa kwenye kikosi cha watu 18,” alisema kocha huyo.

“Alikuwa na tatizo katika mgongo wake lakini alikuwa anaweza kucheza,” aliongeza kocha huyo.

Drogba ambaye aliondoka Chelsea mwezi Julai mwaka jana, amekuwa akitumiwa kama mchezaji wa ziada katika mechi mbili kati ya nne.


Amefunga mabao 10 katika mechi 21 msimu huu.

No comments