KOCHA WA BARCELONA AMWONDOA KIPA MARC ANDRE TER STEGEN KWENYE LAWAMA ZA KUFUNGWA NA CELTA VIGO

KOCHA Luis Enrique amejitwisha zigo la lawama baada ya kusema kuwa ndiye anayetakiwa kulaumiwa kwa kipigo cha hivi karibuni ilichokipata Barcelona cha mabao 4-3 dhidi ya Celta Vigo na wala si mlinda mlango wake Marc Andre ter Stegen.

Makosa binafsi ambayo yamekuwa yakifanywa na raia huyo wa Ujerumani ndiyo yanayodaiwa kuwafanya mabingwa hao kuambulia kipigo cha pili katika michuano hiyo ya La Liga msimu huu.

Hata hivyo kocha huyo wa zamani wa Celta, Luis Enrique anaziondoa lawama juu ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 kutokana na matokeo hayo ambayo yameifanya Barca kushika nafasi ya nne huku ikiwa nyuma kwa pointi mbili dhidi ya vinara wanaoongoza ligi hiyo, Atletico Madrid.

“Kipigo ni kwa ajili ya kila mmoja," kocha huyo alikiambia kituo cha televisheni cha Barca tv.

“Kwanza kwangu mimi ndiye ninatakiwa kubeba lawama kwa ajili ya timu na kwa sasa tunatakiwa kujiangalia wenyewe,” aliongeza kocha huyo.


Alisema kuwa siku hiyo ilikuwa ni nzuri kwao kwani walikuwa na nafasi ya kukaa kileleni mwa Ligi lakini wakashindwa kuitumia.

No comments