MOURINHO AOMBA MUDA ILI KUWASOMA ZAIDI VIJANA WAKE...

KOCHA Jose Mourinho amesema kwamba bado anahitaji muda ili aweze kuwasoma wachezaji wake Manchester United na akasema kuwa anatarajia kukutana na vigingi katika kipindi cha miezi michache ijayo.

Juzi Man United walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Zorya katika michuano ya Ligi ya Europa na huku ikionyesha kiwango cha chini tofauti na ilipoibuka na ushindi wa bao 4-1 dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Leicester City.

Matokeo hayo ndio yaliyokirejesha katika njia nzuri kikosi hicho cha Mourinho baada ya kupoteza mechi mfululizo dhidi ya Manchester City na Watford katika michuano hiyo ya Ligi Kuu England.

“Nahitaji muda, nahitaji wachezaji wacheze. Nahitaji kuwaona katika mazingira tofauti,” alisema Mreno huyo.
“Nahitaji kufahamu mengi kuhusu wao, kuna mambo mengi ya kujifunza kuhusu wachezaji na unapofanya kazi nao kwa muda mrefu ndiyo unavyowafahamu vizuri,” aliongeza Mourinho.

Alisema kwamba, mara zote huwa kuna mambo ambayo huwa yanafichuka nyuma ya wachezaji pindi utakapofanya kazi nao kwa muda wa miezi mitano hadi sita.

No comments