MWANATENISI NOVAK DJOKOVIC ASEMA HAFIKIRII HABARI YA MATAJI KWA SASA

KINARA wa tenisi duniani, Novak Djokovic amesema kuwa hafikirii suala la kunyakua mataji wala kushuka kwenye viwango vya mchezo huo duniani upande wa wanaume.

Mserbia huyo anayekamata nafasi ya kwanza kwa viwango aliyasema hayo mwishoni mwa wiki hii akidai kwamba hataki kujipa presha kwenye maisha yake ya kucheza mchezo huo.

“Sitaki kufikiria suala la kushinda mataji au kuwa namba moja duniani, nataka niepukane na presha,” alisema Djokovic, mshindi wa mataji 12 makubwa ya tenisi.

“Nilijipa presha kubwa baada ya kuibuka bingwa wa Roland Garros mwaka huu na sikulipenda hilo,” aliongeza.

“Mara nyingi huwa nafurahia mchezo lakini katika miezi michache iliyopita yamezungumzwa mengi kwamba nakaribia kuweka historia mpya, hilo limenipa sana presha.”


“Sio kwamba sitashiriki katika mchezo huo, lakini pia nataka nicheze sio tu kwa sababu nahitaji kushinda mataji,” alisema.

No comments