MWANNE WA EAST AFRICA RADIO ALIVYOUCHOKONOA MPAMBANO WA ISHA MASHAUZI NA LEYLA RASHID


MTANGAZAJI wa East Afriaca Radio Mwanne bint Othman Jumapili iliyopita alichokoza moto wa mpambano wa waimbaji wawili nyota wa taarab Isha Mashauzi na Leyla Rashid.

Waimbaji hao wanaumana Jumamosi hii katika ukumbi wa Dar Live Mbagala jijini Dar es Salaam na kusindikizwa na bendi zao za Jahazi Modern Taarab na Mashauzi Classic Modern Taarab.

Kupitia kipindi chake cha Tam Tam za Mwambao kinachoruka kila Jumapili saa nne asubuhi kupitia East Afriaca Radio, Mwanne (pichani juu) akauchokonoa mpambano huo kupitia simu aliyompigia Isha Mashauzi.

Mwanne alimpigia simu Isha Mashauzi ili atoe maoni yake kuhusu tuzo za muziki na filamu – EATV Awards zitakazo fanyika Disemba mwaka huu, lakini akaamua pia kumuuliza kuhusu mpambano wake na Leyla.

Sura ya maongezi ikabadilika, meseji za wasikilizaji nazo zikabadilika na munkari wa onyesho hilo ukatawala.

Isha Mashauzi akasema mashabiki wa Leyla waache woga wa kutaka kumpangia nyimbo za kupiga na kwamba atahakikisha anapiga nyimbo zake zote zinazotesa sokoni kwa hivi sasa ikiwemo “Nimpe Nani”.

Ikumbukwe kuwa Mwanne aliwahi kuwa mwimbaji wa Jahazi na kufanya kazi na waimbaji wote hao wawili ndani ya kundi hilo kabla Isha hajaenda kuanzisha Mashauzi Classic na  huku Mwanne akirejea kwenye kazi ya utangazaji.

No comments