SERGE AURIER AMWAGIWA SIFA KWA KUOKOA MAISHA YA MOUSSA DOUMBIA

BEKI wa klabu ya Paris Saint-Germain kutoka Ivory Coast, Serge Aurier amesifiwa sana baada ya kuokoa maisha mchezaji wa Mali, Moussa Doumbia Jumamosi iliyopita.

Doumbia alianguka na kupoteza fahamu baada ya kukabwa na Lamine Kone wa Sunderland.

Aurier aliingia kati baada ya kuona mchezaji huyo wa Rostov akiwa anatapatapa, akamlaza kwa upande na kumzuia kuumeza ulimi wake.

Meneja wa Mali, Alain Giresse amesema alizungumza na Aurier baada ya mchezo huo na kumshukuru.

“Wachezaji wote waligundua kwamba Doumbia alikuwa anakabwa kooni na kushindwa kupumua na alikuwa karibu kumeza ulimi wake,” Giresse aliiambia radio ya Ufaransa, RMC.

“Ni hapo ambapo Aurier akiwa na mmoja wa wachezaji wetu alichukua hatua haraka wakamlaza upande na kuutoa ulimi wake kwa sababu alikuwa anakaribia kupoteza maisha.” 


Ivory Coast walishinda 3-1 mechi hiyo ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018.

No comments