SIR ALEX FERGUSON AELEZA ANAPOKOSEA MOURINHO KATIKA USAJILI

HUU ni ushauri na somo kuu! Baada ya kimya kingi cha aliyekuwa bosi wa mashetani wekundu, Alex Ferguson, sasa ameweka neno juu ya usajili ujao wa Manchester United.

Kiroho safi Ferguson amemwambia Jose Mourinho kam anataka kuongeza wachezaji kikosini anatakiwa kuacha kabisa kufanya usajili wa kuangalia majina, bali awe mbunifu wa kuangalia aina ya wachezaji wanaoweza kulelewa ndani ya United ili waje kuwa nyota wa baadae.

Ferguson aliyasema hayo katika kipindi hiki ambacho nyota Paul Pogba hajaanza kuonyesha mafanikio yaliyotarajiwa na wengi tangu asajiliwe kwa gharama kubwa.

“Ninaweza nikamwambia jambo moja kocha Jose Mourinho kuwa kama anataka kufanya usajili katika dirisha dogo, basi aachane na usajili wa majina makubwa.”

“Badala yake aangalie wachezaji walio na vipaji lakini wa umri mdogo.”

“Mimi nilifanya hivyo kwa wachezaji engi, akiwemo Ryan Giggs, Rio Ferdnand, Cristiano Ronaldo na hata Wayne Rooney. Ingawa walikuwa hawana majina lakini walikuja kuwa hadhina ya timu.”

“Kisha lazima kocha kama wa United aangalie utamaduni wa soka la England ambao ni lazima kujali zaidi wachezaji wanaoweza kudumu kikosini kwa kipindi kirefu,” alisisitiza.

Kauli ya Ferguson ni kama inaungana na ile ya Arsene Wenger ambaye aliwahi kumweleza aliyekuwa kocha wa mashetani hao kabla ya Mourinho, Van Gaal kuacha kusajili wachezaji kwa kufuata majina.

Van Gaal alitua katika kiti cha moto cha Manchester United msimu wa kiangazi mwaka juzi na mara moja aliingia sokoni kusajili wachezaji wapya saba wenye majina makubwa.

Aliwasajili akina Angel Di Maria, Radamel Falcao, Ander Herrera, Daley Blind, Marcos Rojo na kinda Luke Shaw.

Lakini Ferguson ameongeza kuwa: “Naamini Manchester United wanaangushwa na falsafa ya kutaka kusajili wachezaji wa majina makubwa lakini uwezo wa kuibeba timu ni mdogo.”

“Anachotakiwa kutambua ni kwamba wakati mwingine timu haihitaji kusajili wachezaji kwa sababu ya majina bali ni kutafuta wachezaji vijana na kuwaandaa kama ilivyokuwa kwa akina Giggs, Ferdinand, Ronaldo na Rooney.”

“Wakati ninakuja hapa nilikuwa na timu imara waliyozoea kucheza soka la Ligi ya Premier, lazima Mourinho atambue jambo hilo,” alisisitiza Ferguson.


Aliongeza: “Leo ni kama ilikuwa miaka ile, lazima utambue utamaduni wa soka la namna hii, vinginevyo hutaweza kupata usingizi usiku,” alisisitiza mkongwe huyo.

No comments