VAN PERSIE AMKUMBUKA FERGUSON… asema angekuwepo nae angekuwa bado anakipiga Man United

STRAIKA Robin Van Persie amefunguka akisema kuwa angekuwa bado anakipiga kwenye timu ya Manchester United endapo aliyekuwa kocha wake, Alex Ferguson angekuwa bado anainoa klabu hiyo ya Old Trafford.

Jana staa huyo raia wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 33, alikuwa akirejea kwenye klabu yake ya zamani tangu alipoondoka Julai mwaka jana na kwenda kujiunga na klabu ya Fenerbahce wakati timu hizo zilipokuwa zikikutana kwenye mechi ya Ligi ya Europa.

Katika kipindi cha miaka mitatu aliyoichezea Man United, Van Persie aliweza kuifungia mabao 58 na akafanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England katika msimu wake wa kwanza ikiwa chini ya Ferguson.

Baada ya hapo straika huyo alicheza chini David Moyes na Luis van Gaal kabla ya kuuzwa na anasema kuwa mambo yangekuwa tofauti kama sio Ferguson angeondoka mwaka 2013.

“Huwezi kufahamu,” staa huyo aliwaambia waandishi wa habari bada ya kuhojiwa ni kitu gani kingetokea endapo Ferguson angekuwa bado anaifundisha timu hiyo.


“Ila ninachoweza kusema pengine ningekuwa bado ni mchezaji wa Manchester United. Wakati nasajiliwa sikuwa na mawazo kama Sir Alex angebaki muda mfupi lakini kwenye soka kila kitu huwa kinaweza kubadilika, huwezi kuweka mipango yako binafsi ama kocha unayemtaka,” aliongeza staa huyo.

No comments