ABDUL MISAMBANO AIKATAA KATA KATA TARADANCE


MWIMBAJI nguli wa taarab na dansi Abdul Misambano, amesema hakubaliani hata kidogo na ujio wa “taradance” ndani ya muziki wa taarab.

Akiongea katika kipindi cha Sham Sham za Pwani cha ITV wiki iliyopita, Misambano akaenda mbali zaidi kwa kulaani vikali kitendo cha kuchukua vipande vya nyimbo za dansi na kuviweka kwenye taarab.

Mwimbaji huyo wa TOT akasema kuna aina mbili za taarab – Taarab Asili na Modern Taarab.

“Taradance ni angamizo la muziki wa taarab, sio jambo linaposwa kuungwa mkono, mimi binafsi siikubali hata kidogo taradance,” alisema Misambano wakati akiongea na Hawa Hassan katika mahojiano hayo.

“Mimi niko TOT naimba dansi na taarab, asilimia 70 ya tungo za dansi zinazotamba TOT ni tungo zangu, kama ni kuchanganya vipande vya nyimbo za dansi kwenye taarab basi mimi ningekuwa wa kwanza kufanya hivyo, ningechukua nyimbo zangu za dansi na kuziweka kwenye tungo zangu za taarab, lakini sikutaka kufanya hivyo maana hiyo ingekuwa dalili ya kuishiwa.

“Mtu anachukua kipande cha wimbo wa zamani wa dansi tena ambao wala haumuhusu kisha anauweka kwenye taarab, hii si sawa. Kama unataka kufanya hivyo ni bora uombe idhini ya kufanya ‘remix’ ya wimbo mzima tujue moja”, alitiririka Misambano.

Mwimbaji pia aliwaasa wanamuziki wa taarab wa sasa kuienzi taarab asili kwa kuwa hiyo ndiyo nguzo ya taarab.

“Nashauri bendi zetu za Modern Taarab ziwe zinatunga japo wimbo mmoja wa taarab asilia katika kila albam”, alisema mkali huyo aliyepata umaarufu mkubwa kupitia wimbo wake wa “Asu” zaidi ya miaka 15 iliyopita.

No comments