HARUFU YA UFISADI YAGUBIKA UWANJA WA WESTHAM

VYOMBO vya uchunguzi nchini Uingereza wiki ijayo vitaanza kufanya uchunguzi unaohusiana na kile kinachoitwa harufu ya ufisadi katika ubadilishaji wa uwanja wa Westham nchini humo.

Meya wa jiji la London, Sadiq Khan ameamuru kufanyika kwa uchunguzi juu ya ongezeko la gharama za euro mil 50 wakati wa kubadilisha uwanja wa Westham.

Mwaka 2015 aliyekuwa meya wa jiji hilo, Boris Johnson alisema kuwa kubadilishwa uwanja huo kutoka kuwa uwanja wa Olimpiki hadi kuwa uwanja wa mpira wa miguu kungegharimu pauni mil 272, kiasi ambacho sasa kimepanda hadi kufikia mil 323.

Paul Fletcher ambaye amehusika katika ujenzi wa viwanja zaidi ya 30 anasema ni lazima uwanja huo ujengwe upya kutokana na majukwaa ya mabingwa kuwa mbali sana na uwanja, jambo ambalo halipendezi kwa mchezaji wa mpira wa miguu.

“Hata kama hautazoea kupita katika viwanja vingine lakini muonekano wa majukwaa ya mashabiki ya mashabiki yapo mbali na sehemu ya kuchezea. Hili si jambo zuri na kwa ukweli kama tunaogopa gharama uwanja huu utakuwa kituko,” akasema.

Lakini meya huyo amesema kwamba lazima kufanyike uchunguzi wa kina maana hakuna mahali kokote ambako ameona kuna kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi na hivyo ili kuondoa mashaka ya upigaji wa pesa hizo lazima watu wajiridhishe.


“Kuna mashaka ya rushwa. Lakini pia inabaki kama mashaka tu hadi pale uchunguzi utakapokamilika,” amesema meya Khan.

No comments