JAHAZI MODERN TAARAB YAMSAJILI ALLY JAY … ataanza kuonekana Ijumaa Equator Grill, Jumamosi Lekam Pub, Jumapili Lunch Time Manzese


KUNDI la Jahazi Modern Taarab limezidi kujiimarisha kwa kumsaini mpiga kinanda, mtunzi na mpangaji wa muziki Ally Jay “Mwarabu wa Dubai”.

Ally Jay amesaini kujiunga na Jahazi usiku huu na ataanza kuonekana jukwaani Ijumaa hii ndani ya ukumbi wa Equator Grill Mtoni jijini Dar es Salaam.

Ally Jay pia ataonekana kwenye jukwaa la Jahazi siku ya Jumamosi wakati bendi hiyo itakapotumbuiza katika ukumbi wa Lekam Royal Pub Buguruni na Jumapili hii ndani ya kiwanja cha Lunch Time Manzese.

Mkurugenzi wa Jahazi Khamis Boha amesema wanaendelea kurudisha wasanii wao muhimu waliowahi kuitumikia Jahazi katika vipindi tofauti.

Ally Jay aliitumikia Jahazi miaka sita au saba iliyopita kabla ya kwenda kuanzisha kundi la Five Stars ambalo amedumu nalo hadi leo hii aliporejea nyumbani.

Msanii mwingine wa zamani aliyerejea Jahazi ni mpiga solo maarufu Jumanne Ulaya.

Boha amewataja wasanii wengine waliorejeshwa Jahazi ni pamoja na wale walioihama hivi karibuni ambao ni waimbaji Mwasiti Kitoronto na Fatma Kassim, mpiga bass Mussa Bass  pamoja Mazoea mkali wa kinanda.

Jahazi pia imewasajili wasanii wapya wawili mwimbaji Hadija Mbegu na mpiga kinanda Shaaban Kinanda.

Boha amesema kwa sasa Jahazi imefunga usajili wake kwa upande wa kinanda na gitaa la solo.

“Solo tunao watu wawili Emeraa na Jumanne Ulaya, kinanda tunao watatu Ally Jay, Shaaban Kinanda na Mazoea hivyo hatuhitaji tena mtu mwingine katika upande huo,” alisema Boha.

“Mezani tuna maombi ya kazi kutoka kwa waimbaji watatu wa zamani wa Jahazi, bado tunafikira kama kuna haja ya kuwapokea au la,” aliongeza Boha na kusisitiza kuwa kamwe Jahazi haiwezi kufa.
Ally Jay mwenye jezi ya njano akisaini kujiunga na Jahazi huku viongozi wa Jahazi wakishuhudia

No comments