JOSE MOURINHO KUFUKUZA MASTAA MANCHESTER UNITED

NDANI ya klabu ya Manchester United kuna jambo linakwenda kutokea hivi karibuni linalohusu masuala ya usajili.

Taarifa ni kwamba kocha Jose Mourinho yumo katika mipango ya kuwakataa baadhi ya nyota waliomo kikosini kwa sasa.

Mtandao wa klabu hiyo umebainisha idadi ya wachezaji walio hatarini kukumbwa na panga la usajili ambao ni wanandinga wane na mpango huo umeelezwa kutekelezwa katika kipindi cha usajili wa dirisha la mwezi Januari.

Ndani ya kikosi hicho chenye jumla ya wachezaji 23, kuna majina ya Bastian Schweinsteiger, David de Gea, Sergio Romero na Sam Johnstone ambao wanatajwa kuwemo hatarini kukumbwa na panga hilo.

Wadau wa klabu ya Manchester United wameitaja idadi hiyo kuwa ni kubwa kuwahi kutokea katika kipindi cha hivi karibuni kwa wachezaji kuachwa.

Pamoja na waliotajwa katika orodha hiyo, jina la Wayne Rooney linaangaliwa katika jicho la tahadhari la huenda akaachwa ama kuruhusiwa kuondoka katika viunga vya Old Trafford.

Hata hivyo Mourinho amekuwa akikanusha mara kadhaa juu ya suala la kuachana na Rooney ingawa tayari ameambiwa anaweza kuondoka United.

Mwingine anayeweza kuingia katika kapu la kuachwa ni Morgan Schneiderlin aliyejiunga na United iliyokuwa chini ya kocha Louis Van Gaal.

Schneiderlin tayari amepewa ruksa ya kuweza kuondoka Old Trafford kama mchezaji huru baada ya kushindwa kuwepo kwenye kiwango bora cha kuweza kulishawishi benchi la ufundi la sasa.


Wengine ambao hawana uhakika wa kuendelea kubaki United ni pamoja na Memphis Depay na Matteo Darmian ambao wanahusishwa na kutaka kuhamia katika klabu za nchini Italia.

No comments