KOCHA JURGEN KLOPP ATIMIZA MWAKA MMOJA WA MAFANIKIO LIVERPOOL

MWEZI Oktoba mwaka jana Liverpool ilimtangaza rasmi kocha Jurgen Klopp kurithi mikoba ya Brendan Rodgers. Klopp alikuwa ametoka mapumzikoni baada ya kuachana na klabu ya Borussia Dortmund ambayo aliipa mataji yote muhimu ndani ya Ujerumani.

Mbali na mataji ya ndani, pia kwenye michuano ya Ulaya Dortmund chini ya Klopp ikafika fainali ambayo walipoteza dhidi ya wapinzani wao, Fc Bayern Munich kwenye uwanja wa Wembley.

Ni takriban mwaka mmoja umepita tangu Kloipp aingie kandarasi ya miaka mitatu kuwafundisha majogoo wa Anfield.

Miezi minne tangu alipojiunga na Liverpool, Klopp alifanikiwa ucheza fainali ya Kombe la Ligi bahati mbaya akapoteza dhidi ya City kwa penati 3-1.

Mwezi Mei mwaka huu wakapoteza tena fainali nyingine dhidi ya Sevilla kwenye michuano ya Europa.

Kabla ya hapo Liverpool ilikuwa haijafanikiwa kutinga hatua yoyote ya fainali michuano ya Ulaya tangu mwaka 2007.

Wikiendi hii Liverpool imekaa kwenye kilele cha msimamo wa Ligi kwa mara ya kwanza chini ya Jurgen Klopp.

Kwenye Ligi yenye Pepo Guardiola, Antonio Conte, Maurcio Pochettino, Arsene Wenger na Jose Mourinho sio jambo rahisi.

Liverpool ina wastani mzuri wa mabao hadi sasa, hakuna timu ambayo inaweza kutikisa nyavu za wapinzani mara 30 ukiondoa Liverpool. Timu inacheza soka la uhakika lenye ladha zote, mabao na burudani.

Pointi 26n zimetisha kumweka Klopp kwenye nafasi ya kwanza tangu alipojunga na Liverpool tangu takriban mwaka mmoja uliopita.

Tofauti na msimu uliopita ambao alikuta tayari timu imeshasajiliwa na Rodgers, msimu huu Klopp amefanya usajili mwenyewe na pia ametengeneza aina ya timu anayoitaka mwenyewe. Klopp ni miongoni mwa makocha wanaoonekana kufanikiwa kimfumo msimu huu wa Ligi Kuu nchini Uingereza.

Ana nafasi kubwa ya kuipeleka Liverpool kwenye mafanikio mapya ya kunyakua taji la Ligi Kuu nchini humo ambalo wamelikosa kwa miaka takriban 26.

Pep Guardiola alionekana aipanda na kushuka akiwa na kikosi chake cha Man City. Tayari hadi sasa amepoteza pointi sita baada ya kutoka sare tatu kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Etihad Stadium.

Jose Mourinho bado anajikongoja na kikosi chake cha Manchester United kama ilivyo kwa Mauricio Pochetino ambaye anapoteza pointi nyingi kwa kutoka sare kwenye michezo ya EPL.

Wapinzani ambao wanaweza kuzima ndoto za Klopp ni Antonio Conte ambaye amefanikiwa kuingiza mfumo wake wa Kitaliano maarufu kama “Catenaccio” pale Chelsea.

Mwingine ni Arsene Wenger lakini kwa bahati mbaya huwa anaanza Ligi vizuri na kumaliza vibaya.

Klopp anaweza kuifikisha Liverpool kwenye mafanikio ya kina Bill Shankys. Bahati nzuri Liverpool kwa sasa sio timu ambayo ina presha kubwa kuifundisha kama ilivyo kwa Manchester United na Chelsea.


Huyu ni miongoni mwa makocha ambao wanaweza kukupa mafanikio kwenye timu yako tena kwa kutumia koiasi kidogo tu cha fedha. Baada ya mwaka mmoja tangu ajiunge na majogoo ameshika nafasi ya kwanza kwenye Ligi. Je, ikifika mwezi Mei mwakani atakuwepo tena kwenye nafasi hiyo? Tusubiri tuone.

No comments