KOCHA WA TIMU YA TAIFA YA MAREKANI AFUNGASHIWA VIRAGO

JURGEN Klinsmann ametimuliwa kazi ya kufundisha timu ya taifa ya Marekani baada ya miaka mitano ya kufanya kazi hiyo.

Uamuzi huo ulichukuliwa kutokana na timu hiyo kuboronga kwenye michuano ya awali ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Russia mwaka 2018.

Marekani ilichakazwa mabao 4-0 na Costa Rica ugenini kwenye mechi ya michuano hiyo wiki iliyopita.

Kipigo hicho kilifuatia kingine cha mabao 2-1 ambacho timu hiyo ilipokea kutoka kwa Mexico nyumbani na kufanya ishike mkia kwenye michuano ya awali ya Kombe la Dunia kwa nchi za CONCACAF.

Timu tatu kutoka katika Kundi hilo ndizo zinatakiwa kufuzu kwa mashindano hayo.


Rais wa Shirikisho la Soka la marekani, Sunil Gulati alisema wamefanya uamuzi huo mgumu licha ya ukweli kuwa Klinsmann alifanya mambo mengi mazuri wakati akiinoa timu hiyo.

No comments