MASHUJAA BAND WAINGIA STUDIO KUPAKUA NYIMBO 8 MPYA ...Chaz Baba ndo basi tena


HATIMAYE bendi ya Mashujaa iliyosukwa upya imeingia studio kurekodi ngoma mpya nane.

Mashujaa Band ambayo ilisimamisha maonyesho yake na kuingia kambini kwa zaidi ya miezi miwili, inatarajiwa kurejea ulingoni hivi karibuni kwa kishindo huku ikiwa na sura mpya kabisa.

Bendi hiyo imejitosa katika studio za Soft Records chini ya producer Pitshou Bampadi ambapo Mkurugenzi wa Masoko wa Mashujaa, Maxi Luhanga ameiambia Saluti5 kuwa nyimbo hizo zipo katika miondoko tofauti ikiwemo rumba laini.

Kwenye safu ya waimbaji ukiondoa mwenyeji Pasia, wengine wote ni wapya akiwepo Facebook, John, James, Kandoro na Bob J.

Kwenye safu ya wapiga vyombo kuna vichwa kama Shalamama anayepiga solo, Mellen kwenye rhythm, wakati bass gitaa kuna Kizza Bass na drum zinakung’utwa na Wagadugu.

Miongoni mwa nyimbo zinazorekodiwa ni pamoja na “Fashion ya Mapenzi”, “Nipe Nikupe”, “Huruma” na “Thamani ya Mapenzi”.

Katika ujio huu mpya wa Mashujaa hakuna jina, sauti wala sura ya mwimbaji Chaz Baba ambaye bado yuko kwenye mgogoro wa kimkataba na bendi hiyo.

No comments