MSONDO HII SASA SIFA!!! …YAJA NA SURPRISE YA UJIO WA GWIJI LA MUZIKI AFRIKA MASHARIKI DISEMBA 2 …ni Luza Elias mkali wa ala za upepo


HATIMAYE Msongo Ngoma Music Band imefanya usajili wa kufunga mwaka wakati ikielekea kwenye onyesho la ‘Msondo Familiy Day’.

Onyesho hilo ambalo hufanyika kwa wastani wa mara moja kwa mwezi, safari hii litafanyika Mango Garden Kinondoni Ijumaa ya Disemba 2. 

Hii ni mara ya pili kwa Family Day ya Msondo kufanyika Mango. Mara ya kwanza ilifanyika Septemba 30 mwaka huu.

Katika kuelekea onyesho hilo, bendi hiyo kongwe hapa nchini, imeamua kumsajili mwanamuziki gwiji Afrika Mashariki Luza Elias (pichani juu) ambaye ni bingwa wa kupiliza saxophone.

Kati ya mwaka 1970 hadi 1992, Luza Elias alitamba na bendi kadhaa zikiwemo Jamhuri Jazz ya Tanga, Simba Wanyika na Mwenge Jazz kabla ya kwenda kufanya muziki nchini Marekani alikodumu kwa miaka 16.

Kuingia kwa Luza kunakuja kufunika pengo la mpiga saxophone ndani ya Msondo tangu alipoondoka Shaaban Lendi.

Mmoja wa waratibu wa onyesho hilo, Abdulfareed Hussein, ameimbia Saluti5 kuwa Msondo Family Day ya Disemba 2 ndiyo ya mwisho kwa mwaka huu na ndiyo maana onyesho hilo linakuja na mshindo mkuu ikiwemo usajili huo wa Luza Elias.

“Hii ndiyo Msondo Family Day ya kufunga mwaka, hatutakuwa na Family Day nyingine mwaka huu,” alisema Abdulfareed.

Kama ilivyo ada, dhumuni la ‘Msondo Family Day’ ambayo ni kuongeza mshikamano baina ya wanamuziki wa Msondo, mashabiki na wadau wakubwa wa bendi hiyo ikiwa ni pamoja na kupeana zawadi mbali mbali.

No comments