MTAALAM CRISTIANO RONALDO AENDELEA KUZOA TUZO

NEEMA imeendelea kumshukia mshambuliaji na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa Ligi ya nchini Hispania kwa msimu uliopita kupitia tuzo za gazeti la Marca.

Ronaldo ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo ikiwa ni siku moja baada ya kukamilisha mpango wa kusaini mkataba mpya ambao utamweka Santiago Bernabeu hadi mwaka 2021.

Ronaldo ameshinda tuzo hiyo kufuatia uwezo mkubwa ambao aliuonyesha katika kikosi cha Real Madrid, jambo ambalo lilitoa msukumo kwa wahusika kumpigia kura zaidi tofauti na wapinzani wake.

Ronaldo alifunga mabao 35 na kutoa pasi 11 za mwisho zilizosaidia ushindi kwa klabu yake katika michezo ya Ligi lakini hatua ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Ulaya pamoja na kuiwezesha kutwaa Kombe la Euro 2016 nayo imeonyesha kuchangia mafanikio anayoendelea kuyapata.

Tuzo aliyotwaa mshambuliaji huyo kwenye umri wa miaka 31 inaitwa “Alfredo di Stefano” jina la aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid.

Hii inakuwa mara ya nne kwa Ronaldo kutwaa tuzo hiyo, tofauti na mpinzani wake wa karibu, Lionel Messi ambaye ameshatangazwa kuwa mshindi mara tano kwa misimu ya 2008/09, 2009/10, 2010/11 na 2014/15.

Tuzo ya kocha bora wa msimu iitwayo “Miguel Munoz” ilikwemnda kwa meneja wa klabu ya Atletico Madrid, Diego Simeone.

Huku Asier Garitano akichukua tuzo ya kocha bora wa Ligi Daraja la Kwanza. Alvaro Morata ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji aliyechangia mafanikio ya timu ya taifa.


Sherehe za utoaji wa tuzo hizo zilihudhuriwa na wageni mashuhuri kama rais wa La Liga, Javier Tebas, Emilio Butragueno, Fernando Hierro, rais wa atletico Madrid, Enrique Cerezo pamoja na mtendaji mkuu wa Sevilla, CF Jose Castro.

No comments