OZIL AKUMBUKA UJERUMANI WALIVYOWALIZA BRAZIL KOMBE LA DUNIA MWAKA 2014

KUMBUKUMBU za fainali za Kombe la Dunia la mwaka 2014 zitaendelea kubaki vichwani mwa watu wengi sana kutokana na kile kilichotokea kwenye mchezo wa nusu fainali kati ya Brazil na Ujerumani.

Brazil ndio walikuwa wenyeji wa michuano hiyo na walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kutwaa Kombe hilo kwa mara ya sita.

Hata hivyo, ndoto yao ya k,ubakisha Kombe hilo iligeuka shubiri baada ya kukumbana na kadhia kutoka kwa Ujerumani mnamo Julai 8.

Brazil walijikuta wakipata dhoruba kipindi cha mwanzo baada ya kuruhusu mabao matano ndani ya dakika 18 na kujikuta wakiwa nyuma kwa mabao 5-0.

Haikuwa fedheha tu ya kushindwa kubakisha Kombe hilo kwenye ardhi ya nyumbani bali pia ilikuwa ni aibu mbele ya ulimwengu.

Ujerumani badare waliongeza mabao mawili kipindi cha pili, kabla ya Oscar kuifungia Brazil bao moja dakika ya 90 na kufanya matokeo kuwa 7-1.

Mchezo huo uligusa hisia za mashabiki wengi na kutoa taswira tofauti kabisa. Wachezaji wa Brazil walibaki wakibubujikwa na machozi huku wenzao wa Ujerumani wakiwa na nyuso zilizojaa furaha na bashasha isiyo na kifani wakati huohuo wakiwaonea huruma wenzao.

Hiyo ndiyo hali iliyomkuta nyota wa Arsenal, Mesut Ozil. Ozil ameikumbushia hali hiyo na kusema kuwa alijisikia vibaya kuona Wabrazil wakiwa na majonzi makubwa, hali iliyosababisha kumwambia maneno ya faraja David Luiz baada ya mchezo.

“Wachezaji wote pamoja na mimi mwenyewe tulijawa na mshangao kwa kilichotokea. Lakini baada ya dakika 20 tukawa mbele kwa mabao 4-0, unaweza kuona maajabu hapo,” alisema.

Kama unapoteza mchezo mkubwa kama ule kwenye ardhi ya nyumbani na unaona watu wanalia kama vile, hata wewe utajikuta unaingiwa na majonzi.”


“Hivyo nilichokifanya ni kwenda kwa David Luiz na kumwambia, ‘naomba radhi mna nchi nzuri na watu wazuri pia’.”

No comments