TANZANIA KUSHIRIKI MISS AFRICA …Nape Nnauye akabidhi bendera kwa Julitha Kabete


WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye ametoa baraka zake kwa mwakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya urembo ya Afrika ‘Miss Afrika’ yatakayofanyika, nchini Nigeria.

Katika shindano lililopangwa kufanyika Novemba 28, Tanzania itawakilishwa mshindi wa nne wa michuano ya Miss Tanzania 2016,      Julitha Kabete.

Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Waziri Nape Nnauye alisema serikali imetoa baraka zake kwa mrembo huyo kwa kuwa wanaamini ni shindano zuri litakaloweza kuitangaza vema Tanzania hasa kupitia kauli mbiu ya shindano hilo ambayo inahusu mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

“Tumeingia kusapoti kwa sababu tunataka kuipeleka Miss Tanzania kwenye kiwango kingine licha ya changamoto nyingi ambazo kwa sasa wanakabiliwa nazo,”alisema Waziri Nnauye.

Alisema anafahamu kuwa shindano la Miss Tanzania kwa sasa linakabiliwa na changamoto kubwa ya kurejesha imani kwa baadhi ya wadau hususani wadhamini baada Serikali kufungia Shindano hilo.

“Mimi niwatoe wasiwasi watanzania kuwa kwa sasa mambo yanaenda vizuri na ndio maana mnaona hata sasa hivi tunamsapoti mrembo huyu ambaye ataiwakilisha nchi, hivyo nitoe rai kwa kampuni na taasisi mbalimbali kurejesha imani yao katika shindano hili,” alisema Waziri Nnauye.

Alisema anafurahi kuona kuwa hata mshindi namba nne wa shindano la Miss Tanzania anapata fursa ya kuwakilisha nchi kwenye michuano mikubwa kama ya Miss Afrika,  tofauti na awali ambapo mshindi aliyekuwa akitambuliwa alikuwa ni mshindi wa kwanza pekee.

Alisema anaimani warembo hao watakapotumiwa vizuri watapata fursa ya kuwa mabalozi wazuri kwa nchi yao hivyo amemtakia kila la kheri mrembo Julitha aweze kuiwakilisha vema na hatimae kutwaa taji la Afrika.

Mrembo huyo ambaye anakwenda nchini Nigeria chini ya uangalizi wa Miss Tanzania ,wa mwaka 2001 Millen Magese, ameahidi kuiwakilisha vema nchi kwenye michuano hiyo mikubwa huku akiwaomba watanzania wampigie kura ili aweze kushinda shindano hilo.

Mshindi katika shindano hilo ataondoka na kitita cha dola 25,000 zaidi ya sh. milioni 50 pamoja na gari , mshindi wa pili dola ya KImarekani 15,000  ni sawa na sh.milioni 32 za Kitanzania na wa tatu  dola 10,000 ni sawa na sh.milioni 22.


No comments