VAN PERSIE AWAONDOA HOFU MASHABIKI KUTOKANA NA MAJERUHI YAKE YA JICHO

MWANASOKA maarufu duniani, Robin Van Persie amewaondoa hofu na wasiwasi mashabiki wake baada ya kupata jeraha baya la jicho katika mchezo wa Jumapili ya wikiendi iliyopita.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal na Manchester United alipata ajali kwenye jicho lake katika kipindi cha kwanza kwenye mchezo kati ya Fenerbahce na Akhisar Belediyespor, hali iliyomlazimu kukimbizwa hospitali kutokana na kutokwa damu nyingi sana.

Mapema kabla ya jeraha hilo, alikuwa tayari amefunga bao lakini tukio hilo lilimfanya kutoendelea na mchezo.

Lakini juzi nyota huyo ameandika kwenye ukurasa wake kwamba mashabiki wake wasiwe na hofu kwasababu anaendelea vizuri kabisa.

“Nawashukuru kwa maombi yenu kutokana na jeraha ambalo nimelipata. Baada ya kuletwa hospitali, madaktari wamefanya uchunguzi na wamenihaikishia kwamba jicho langu liko salama,” ameandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

“Awali nililia sana baada ya kupata jeraha, nilijua huo ndio mwisho wangu lakini namshukuru Mungu jicho halijapata madhara. Ninachoweza kusema huu ndio mpira,” akasema.


Amesema kwamba nje ya matibabu hayo, anashukuru kwamba timu yake imekuwa ikipata mafanikio na hilo ndilo kubwa kwake.

No comments